Hii hapa orodha ya mabasi 35 ya Kilimanjaro Truck Company Limited (Kilimanjaro Express) yaliyositishiwa leseni na LATRA kuanzia kesho Jumatatu ya Januari 8,2024

NA GODFREY NNKO

MAMLAKA ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani imefanya ukaguzi wa kushtukiza kwa mabasi ya masafa marefu ili kutathimini hali ya usafiri nchini Januari 6, 2024.



Katika ukaguzi huo wasimamizi wawili wa kampuni ya mabasi Kilimanjaro Express waliwekwa mbaroni kwa kosa la kuzidisha nauli kinyume na iliyoidhinishwa na mamlaka pamoja na kutoa tiketi zisizo za kielekroni.

Aidha,LATRA imeyasimamisha magari yote ya Kampuni ya Kilimanjaro Express kutoa huduma ya usafirishaji kuanzia Jumatatu kutokana na kukiuka masharti ya leseni ikiwemo kutotoa tiketi ya kielektroniki na kuzidisha nauli kwa abiria.

Mkurugenzi Mkuu wa LATRA,CPA Habibu Suluo aliyasema hayo baada ya kufanya ukaguzi wa kushtukiza katika Stendi ya Kimataifa ya Mabasi ya Magufuli na ofisi za mabasi ya kampuni hiyo ya Kilimanjaro zilizopo Shekilango jijini Dar es Salaam.

CPA Suluo alisema, mabasi hayo pekee ndio bado yanatoa tiketi zisizo za kielektroniki na kwamba yamebainika kukiuka masharti mengi ya leseni licha ya kuonywa mara kwa mara na kutozwa faini.

Akizungumza na wasafiri baada ya ukaguzi wa kushtukiza uliofanywa na LATRA kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani kote nchini, CPA Suluo alimesema kuwa, mamlaka imefikia hatua hiyo baada kampuni hiyo kufanya makosa hayo kwa kujirudia bila kubadilika.

“Disemba 22, 2023 timu ya ukaguzi tulipita hapa usiku na kukuta abiria wametozwa TZS. 44,000/= badala ya TZS. 42,000/= iliyoidhinishwa, pia walikuwa hawatoi tiketi za kielekroni, tuliwaonya na kuwaamuru wawarudishie abiria kiasi kilichozidi na wakafanya hivyo.

"Lakini leo tukiwa kwenye ukaguzi wa kushtukiza tumebaini wakiendelea na makosa yaleyale ndio maana kwanza tumewapeleka Polisi na mpaka kufikia Jumatatu Januari 8, 2024 hawatasafirisha abiria kama watakuwa hawajaanza kutumia tiketi za kielekroni,” amesema CPA. Suluo.

Aidha, CPA Suluo amewahimiza wamiliki wa shule zenye mabasi ya shule kuhakikisha leseni zao ni hai na magari yao ni salama kabla ya kufungua shule ili kuhakikisha usalama wa safari na wanafunzi kwa jumla.

“Magari ya Shule yanapewa leseni na LATRA baada ya kukaguliwa kwa kina na Jeshi la Polisi, ndio maana unaweza kuona hakuna matukio mabaya ya magari ya shule kwa upande wa ajali zaidi ya lile la Mtwara na lenyewe lilikuwa halijakaguliwa.

"Kwa hiyo niwahimize wamiliki wa shule kabla ya Jumatatu ambapo shule zinafunguliwa magari yao yawe yamekaguliwa na yana leseni hai ya LATRA, sisi tutapita mitaani kifanya ukaguzi, hivyo ili kuepusha usumbufu usio wa lazima tufuate matakwa ya Kisheria,” ameongeza CPA Suluo.

Kwa upande wake, SACP Ramadhani Ng’anzi, Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani amewataka wasafirishaji kufuata matakwa ya kisheria ikiwa ni pamoja na masharti ya leseni zao sambamba na wamiliki wa Shule kuhakikisha magari yao yanakaguliwa ili kuboresha huduma za usafiri nchini.

“Tunapokea taarifa kutoka kwa raia wema kuhusu wasafirishaji wanaokiuka masharti ya leseni, mfano mzuri ni hii kampuni ya Kilimanjaro ambayo katika ukaguzi wetu tumebaini anazidisha nauli ndiyo maana msimamizi wa kituo hiki na msaidizi wake tumewaweka chini ya ulinzi.

"Hivyo nitoe wito kwa wasafirishaji kufuata sheria za nchi ili kuepuka usumbufu usio wa lazima, na wamiliki wa shule ni vyema  kufuata sheria ambazo zinatuongoza sisi sote ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wana magari mazima, salama na yaliyokaguliwa na kutoruhusu aina yoyote ya burudani,” amesema SACP Ng’anzi.

Naye Bi. Pendo Dosta, abiria aliyezidishiwa nauli ameishukuru Mamlaka kwa kazi nzuri inayoifanya hasa ya kutetea abiria ambapo yeye alirejeshewa nauli yake katika ukaguzi huo, pia ameipongeza Mamlaka na Jeshi la Polisi kwa kuendesha zoezi hilo kwa weledi na ufanisi.

“Nimefurahi sana mmekuja hapa kutusaidia, kiukweli sisi wananchi tulikuwa tunanyanyasika sana, na tulikuwa hatuna budi kulipa kiasi kilichozidi kwa sababu tulikuwa hatujui nini cha kufanya na tunaitaka safari.

"Mimi namshukuru sana Rais wetu Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na viongozi wengine wote, kwa hili la leo nimeamini kuwa wanatuona na wanatusaidia,” amesema Bi. Pendo.

Kufuatia ukaguzi wa kushtukiza uliofanywa na LATRA pamoja na Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani na kubaini kutobadilika na kujirudia kwa makosa kwa kampuni ya Kilimanjaro Express yenye mabasi 35, LATRA imeifungia kutoa huduma ya usafiri kampuni hiyo kuanzia Jumatatu Januari 8, 2024 mpaka pale itakapoonesha utayari wa kufuata masharti ya Leseni kwa Mujibu wa Sheria.

Mabasi 35 ya Kampuni ya Kilimanjaro Express yaliyofungiwa ni T165DMH, T491ARB, T772ADJ, T830AXR, T676DHY, T805DDB, T689DHY, T893APD, T814BGZ, T545BHY, T639AQN, T278ALQ, T860BVA, T708DGQ, T163DMH, T540AQK, T675DHY, T705DGQ, T855AXR, T804DDB, T895APD, T709DGQ, T622DPT, T983AWY, T904ACN, T546BHY, T178EAU, T176EAU, T173EAU, T177EAU, T832ASM, T434DKL, T809BGZ, T871BVA na T706DGQ.

LATRA ni mamlaka ya Serikali iliyoanzishwa kwa Sheria ya Bunge Namba 3 ya mwaka 2019.

Sheria hii ilifuta Sheria ya iliyokuwa Mamlaka ya Udhibiti wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA).

Aidha,LATRA imepewa jukumu la kudhibiti sekta ya usafiri ardhini, hususani usafiri wa mizigo na abiria.

Usafiri ambao unajumuisha mabasi ya njia ndefu, mabasi ya mijini, magari ya mizigo, teksi, pikipiki za magurumu mawili na matatu, usafiri wa reli na usafiri wa waya.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news