NA DIRAMAKINI
JESHI la Zimamoto na Uokoaji limesema, katika kipindi cha Januari hadi Disemba, 2023 walikabiliana na matukio ya moto 2,076 ambayo yalisababisha vifo vya watu 38 na majeruhi 146, ukilinganisha na matukio hayo katika kipindi cha mwaka uliopita 2022, ambapo kulikuwa na matukio ya moto 1,854 vifo vya watu 32 na majeruhi 66.
"Jeshi linawajulisha kuwa katika kipindi cha mwaka 2023, lilikabiliana na matukio ya majanga ya moto, ajali za barabarani, uokoaji nchi kavu na majini.
"Pia tumeendelea kufanya ukaguzi wa kinga na tahadhari dhidi ya majanga, kutoa elimu kwa umma pamoja na kufanya uchunguzi wa majanga mbalimbali.
"Tulifanikiwa kutoa huduma za uokoaji katika maeneo 1,195, matukio hayo yalisababisha yifo 684 na majeruhi 1,465, ukilinganisha na matukio ya uokoaji 567, vifo na majeruhi 1,010 mwaka uliopita 2022. Aidha tunatoa pole kwa wote waliopoteza ndugu na jamaa zao katika majanga hayo;
Hayo ni kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari ambayo imetolewa leo Januari 2024 na Msemaji wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji makao makuu Dodoma,SACF Puyo Nzalayaimisi.
Amefafanua kuwa, jumla ya maeneo 12,382 yalipatiwa elimu moja kwa moja na maafisa na askari wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ukilinganisha na maeneo 7,511 yaliyofikiwa mwaka 2022.
Msemaji huyo amebainisha kuwa, elimu hiyo ilitolewa kupitia vyombo vya habari ambapo walifanya vipindi 728, ikiwa vipindi 606 vya redio na 122 vya runinga, ukilinganisha na vipindi 602 vilivyofanyika mwaka 2022 ikiwa redio ni 467 na runinga 135.
"Katika ukaguzi wa kinga na tahadhari dhidi ya majanga ya moto tulifanikiwa kuyafikia maeneo 61,424 ambayo yalifanyiwa ukaguzi ukilinganisha na maeneo 42,858 mwaka 2022, michoro ya ramani za majengo 2,431 zilipitishwa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji na kupata ushauri wa kitaalam ukilinganisha na michoro ya ramani za majengo 297 mwaka uliopita 2022.
"Tunauhakikishia umma tutaendelea kufanya ukaguzi wa kinga na tahadhari dhidi ya majanga ya moto, kutoa elimu kwa umma, kushirikiana na Halmashauri za Miji na Majiji ili kuhakikisha tunapanga Miji yetu ili iwe salama wakati wa majanga na kuliwezesha jeshi kutoa huduma kwa wananchi kwa wakati bila kuwa na vikwazo vyovyote.
"Tunatoa rai kwa wananchi wote kutoa taarifa mapema wanapoona viashiria au tukio la moto au ajali ya barabarani ikiwa kuna uhitaji wa huduma ya uokoaji, wasisite kupiga namba yetu ya dharura ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji 114 ambayo ni bure kabisa."
Katika hatua nyingine, jeshi hilo limeishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Dkt.Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, kwa kuendelea kuwazesha na kuliongezea nguvu kazi.
Sambamba na kupandisha vyeo vya maafisa na askari na kuliwezesha fedha za miradi ya maendeleo ili kuongeza na kupanua wigo wa upatikanaji wa huduma zake kwa wananchi. "Zimamoto na Uokoaji “Okoa Maisha na Mali Piga namba 114.”