Kishindo cha utekelezaji wa Ilani Jimbo la Ruangwa,Waziri Mkuu aeleza,Kinana aunga mkono

LINDI-Ili kiongozi yeyote afanikiwe kutimiza wajibu na dhamiya ya kuwatumikia wananchi wake na kuwaletea maendeleo ni lazima awe na watendaji au wasaidizi walio tayari kutekeleza majukumu yao wakati wowote na kwa kuzingatia weledi na uaminifu.

Dhamira hiyo ndiyo inayoelezwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa katika kuhakikisha anamsaidia kamilifu Mheshimiwa Rais Dk. Samia Suluh Hassan ili malengo yake ya kuwaletea maendeleo Watanzania na nchi kwa ujumla yanafanikiwa kwa asilimia 100.

“Wananchi wa Ruangwa tutafanya kazi usiku na mchana, wakati wa jua kali na wakati wa mvua kali kuhakikisha tunamsaidia Mheshimiwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ili atekeleze yale ambayo amepanga kuyafanya kwa Watanzania,” alisema.
Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo Januari 2, 2024 kwenye Ujanja wa Likangara wilayani Ruangwa, alipowasilisha taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Jimbo la Rangwa mkoani Lindi kwa kipindi cha miaka mitatu (2020-2023).

Mheshimiwa Majaliwa aliwasilisha taarifa hiyo katika Mkutano Mkuu Maalumu wa CCM Wilaya ya Ruangwa ambapo mgeni rasmi alikuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Ndugu Abdulrahman Kinana. Mkutano huo ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa CCM.

Waziri Mkuu alisema Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameliwezesha Taifa kuendelea kuwa na utulivu, maelewano na mshikamano, hivyo kuwawezesha wananchi kuendelea kushiriki ipasavyo katika shughuli mbalimbali za kijamii.

Mheshimiwa Majaliwa alitumia fursa hiyo kuishauri Kamati Kuu ya CCM (CC) na Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) kutoa fomu moja kwa nafasi urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 na fomu hiyo ni ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Waziri Mkuu alitoa ushauri huo kutokana na uongozi bora na utekelezaji wa Ilani unaofanywa kwa vitendo na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ni Mwenyekiti wa CCM Taifa. Alisema Mheshimiwa Rais mbali na kutekeleza ilani kwa vitendo, pia ameendelea kuwatumikia Watanzania na kuwaletea maendeleo bila ya ubaguzi wowote.

Alisema kwa upande wa wananchi wa Ruangwa wamejipambanua kwa kuishukuru Serikali kwa vitendo kwa kufanya kazi kwa bidii na maarifa kuhakikisha Ilani ya Uchaguzi ya CCM inaendelea kutekelezewa kama ilivyokusudiwa.

DKT. SAMIA AMEFANYA MAMBO MAKUBWA

Pia, Waziri Mkuu alitaja baadhi ya masuala makubwa ya kitaifa yaliyofanywa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan tangu alipoingia madarakani ikiwemo kuendeleza miradi ya kielelezo na ya kimkakati ukiwemo ujenzi wa Bwawa la kuzalisha umeme la Mwalimu Nyerere, ujenzi wa Reli ya Kiwango cha Kimataifa (SGR) na madaraja makubwa.

Kwa upande wa Wilaya ya Ruangwa, Waziri Mkuu Majaliwa alitaja baadhi ya mafanikio yaliyopatikana tangu Serikali ya Awamu ya Sita ilipoingia madarakani ni pamoja na uboreshwaji wa huduma za kijamii zikiwemo za afya, elimu, maji, miundombinu ya barabara na kilimo, hivyo kuwawezesha wananchi kupata maendeleo.

Akizungumzia huduma za afya, Waziri Mkuu alisema serikali imewezesha ujenzi wa hospitali ya wilaya; ujenzi wa vituo vya afya vipya vinne katika kata za Malolo, Nangurugai, Narungombe na Namichiga; ujenzi wa zahanati mpya tisa za Namungo, Mbangara, Muhuru, Namkatila, Mkaranga, Mihewe, Lipande, Mkutingome na Mtakuja na hivyo kuwawezesha wananchi kupata huduma karibu na makazi yao na kwa wakati.

Mheshimiwa Majaliwa amesema mbali na uboreshaji mkubwa uliofanyika katika sekta za afya na elimu, pia imefanyika hivyo katika miundombinu ya usafiri na usafirishaji ambapo kwa sasa wilaya inaendelea na ujenzi wa barabara ya Nanganga-Ruangwa yenye urefu wa kilometa 56. Barabara hii ni mhimili na mkombozi kwa shughuli za kiuchumi kwa Ruangwa.

Aidha, wilaya hiyo inaendelea kutekeleza miradi mikubwa ya maji vijijini ukiwemo ujenzi wa mradi wa kimkakati wa kutoa maji kutoka chanzo cha Chiuwe/Nyangao hadi Ruangwa Mjini wenye thamani ya shilingi bilioni 119 ambao utahudumia vijiji 34 katika Wilaya ya Ruangwa na vijiji 21 vya wilaya ya Nachingwea. Uwekezaji huo utaboresha upatikaji wa maji katika vijiji na kufanikisha upatikanaji wa huduma hiyo vijijini kufikia asilimia 72.01 na mjini asilimia 77.

Pia, Mheshimiwa Majaliwa alisema serikali imefanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya michezo ukiwemo ujenzi wa uwanja wa mpira wa miguu wa Majaliwa na hivyo kuongeza hamasa ya vijana kujihusisha na michezo ambayo ni chanzo cha ajira na kuwapatia burudani. Kwa sasa wilaya hiyo ina timu tatu ambazo ni Namungo inayoshiriki Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara, Namungo B na Ruangwa Queens.

KINANA AMWAGA SIFA

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Ndugu Abdulrahman Kinana alisema maendeleo makubwa yanayoendelea kufanyika wilayani Ruangwa yanatokana na kazi nzuri inayofanywa na Mbunge wa Ruangwa na Waziri Mkuu, Mheshimiwa Majalwa ambaye amekuwa kiungo cha karibu anayewaunganisha wananchi, viongozi wa Chama Cha Mapinduzi na viongozi wa serikali.

Alisema kasi kubwa ya kupeleka maendeleo inayofanyika Ruangwa ni ya kupigiwa mfano, hivyo aliwasihi wananchi kuendeleza umoja na mshikamano katika kujiletea maendeleo ya kweli. “Nampongeza Waziri Mkuu kwa uungwana wake na unyenyekevu wake. Waziri Mkuu ni mtu mtaratibu na muungwana na ndizo sifa ambazo kiongozi anatakiwa awe nazo,”

“Mimi nitakuwa shahidi wa kusimulia kazi nzuri ya maendeleo inayofanywa Ruangwa. Mimi natembea mara nyingi nchi nzima, nimewahi kupita Ruangwa miaka ya 1980 na 2000 lakini Ruangwa ya leo ni tofauti kabisa na Ruangwa niliyowahi kuiona huko nyuma. Nakupongezeni Wana-Ruangwa kwa umoja na mshikamano wenu,” alisisitiza.

Pia, Ndugu Kinana alitumia fursa hiyo kuipongeza Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kufikisha maendeleo katika maeneo mbalimbali na kumfanya avunje rekodi kwa kufikisha fedha nyingi za maendeleo katika halmashauri zote nchini. “Ndugu zangu sifa mnazompa Rais anastahili kwa kuwa anafanya kazi nzuri ya kuwaletea maendeleo Watanzania.”

Katika hatua nyingine, Makamu Mwenyekiti Ndugu Kinana alisema hakuna dhambi yoyote kwa kiongozi aliyeko madarakani anapomaliza awamu ya kwanza kupewa awamu ya pili aendelee kuongoza. “Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan yuko awamu ya kwanza, kwa nini asipewe awamu ya pili? Hakuna sababu ya kusema hapana.”

Aliogeza kuwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia anaonesha njia kwa kupanga, kutafuta mikakati na kuweka vipaumbele na sasa Watanzania wanajivunia mafanikio na hata wana CCM wanaposema mgombea tuliyenaye anatosha kugombea mwaka 2025 nadhani wana hoja hususan kwa kutambua mchango wake mkubwa katika Taifa hili.

Kwa upande wao, wananchi wa Ruangwa wakizungumzia utekelezaji wa Ilani katika wilaya yao walisema wameridhishwa na kasi ya ujenzi wa miradi ya maendeleo na kwamba wanamshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uongozi mahiri, hivyo waliahidi kuendelea kumuunga mkono.

Wananchi hao walisema awali katika wilaya yao kulikuwa na changamoto mbalimbali zikiwemo za upatikanaji wa huduma bora za afya ambapo kwa sasa imekuwa historia baada ya Rais kuidhimisha fedha kwenda Ruangwa na kufanikisha ujenzi wa hospitali ya wilaya, vituo vya afya na zahanati. “Kwa sasa hatuna tabu ya kutembea umbali umrefu kufuata huduma za afya, kila kitu tunakipata hapa hapa hadi operesheni,” alisema Tabia Juma mkazi wa Kata ya Narungombe.

Naye Mzee Abdallah Mtumbe mkazi wa kata ya Nandagala kijiji cha Nandagala ‘A’ alisema kutokana na kazi nzuri ya utekelezaji wa Ilani inayofanywa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na mbunge wa jimbo lao Mheshimiwa Majaliwa hakuma atakayewaambia lolote dhidi ya viongozu hao wakamsikiliza. “Hatuwezi kuwaacha hawa wote wakati wowote, tumeona utekelezaji wa ilani na maendeleo hapa wilayani, nani anaweza kuyafanya haya yaliyofanyika hapa Ruangwa? Alihoji.

Mwananchi mwingine Mwajuma Makota mkazi wa kata ya Nambilanje kijiji cha Nanjaru alisema kwa sasa katika kitongoji chao cha Kiperembende watoto wanasoma karibu na makazi yao baada ya ujenzi wa shule ya msingi kukamilika na hivyo kuwapunguzia kutembea umbali wa zaidi ya kilomita 10 kwenda katika kijiji cha Nanjaru walikokuwa wakisoma awali.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news