NA GODFREY NNKO
BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imewataka wananchi wote na taasisi mbalimbali ambazo zimetunza sarafu za shilingi 50, shilingi 100 na shilingi 100 katika majumba yao, ofisini, magari, vibubu na hawazitumii kuzipeleka katika benki za biashara au kwao ili ziweze kuchambuliwa na kuingizwa katika mzunguko.
Wito huo umetolewa leo Januari 9, 2023 na Meneja wa Idara ya Sarafu wa BoT, Bw. Ilulu Said kwenye semina ya siku moja kuhusu Mfumo Mpya wa Uandaaji wa Sera ya Fedha (Interest Rate-Based Monetary Policy Framework) na Ukusanyaji wa Sarafu.
Semina hiyo imeandaliwa na BoT kwa wahariri wa habari za biashara na uchumi huku ikifanyikia kwenye ukumbi wa benki hiyo jijini Dar es Salaam.
"Benki Kuu ina jukumu la kuhakikisha inatengeneza na kusambaza sarafu katika nchi hii ya Tanzania, kwa maana ya noti na sarafu zake.
"Na tunatakiwa kuwa na uwiano unaoendana sawa sawa, kwa hiyo kama tunavyofanya matengenezo ya sarafu zetu, tunaangalia, nyingi kabisa wote mnaona..elfu kumi, kumi...zinakuwa nyingi, hii ndiyo noti yetu ya juu kabisa katika nchi hii.
"Inafuatiwa na elfu tano, inafuatiwa na elfu mbili na elfu moja. Kwa hiyo zote unapozitengeneza katika yale makadirio zinakuwa na uwiano kwamba nyingi kabisa zinakuwa elfu kumi, zinafuatia elfu tano, zinakuja elfu mbili mpaka zinafika elfu moja.
"Kwa hiyo, uwiano unakwenda hivyo hivyo kadri tunavyokwenda chini, kwa maana kwamba utatengeneza sarafu za 50 si nyingi kama zilivyo za shilingi 100 na shilingi 100 hazitakuwa nyingi kama zilivyo za shilingi 200.
"Hivyo hivyo tutatengeneza sarafu za 200 si nyingi kama zilivyo sarafu za shilingi 500, kwa hiyo tunakwenda hivyo, hata noti zinatumia uwiano.
"Kwa hiyo hata tunapofanya usambasaji sasa, kwa sababu jukumu la kusambaza tunalo, tunasambaza kwa uwiano huo huo.
"Ukienda benki unataka kutoa shilingi bilioni moja mfano hautapewa sarafu labda za shilingi 500, hiyo haiwezekani, watakupa katika uwiano mzuri.
"Kunakuwa na uwiano mzuri, kwa hiyo zote za chini katika hali halisi ya matumizi tunasema ni chenj, shilingi 50 ni chenji hauwezi kubeba kifuko cha shilingi 50 unaenda dukani unataka kununua kitu, haiwezekani, kwa hiyo zenyewe zina-save tu katika uchumi wetu,"amefafanua Ilulu Said.
Amesema, katika kutengeneza sarafu hizo wanaendelea kutekeleza jukumu hilo kikamilifu na kuzisambaza kupitia benki za biashara hapa nchini. "Kwa hiyo hao (benki za biashara) ndiyo wasambazaji wetu kwenda kwa wananchi."
Wakati huo huo, Ilulu amefafanua kuwa, kwa sasa kampeni ya ukusanyaji sarafu inahusisha shilingi 50, 100 na 200 ili ziweze kuingizwa katika mzunguko ziendelee kuwahudumia wananchi.
Amebainisha kuwa,walifanya uchunguzi wakabaini kuwa kwenye mzunguko sarafu hazikuwa za kutosha kwenye uwiano huo ambao wanaufanya katika makadirio yao ya manunuzi na usambazaji.
"Sasa, tukagundua usambazaji umekwenda vizuri kwa sababu tuliagiza kama mnavyoona kwenye tangazo letu hapa, tuliagiza wenzetu wa biashara mwaka 2019 ilifika uwiano wa sarafu kwa maana ya kwenye mzunguko hamna kabisa, kila ukienda unaambiwa ni noti.
"Lakini, sisi tumeagiza wasambaze ziende ziwafikie wananchi, kwa hiyo tarehe 4, Julai, 2019 tukaagiza benki zote wahakikishe wanasambaza na wanafungua madirisha kwenye benki zao kwa ajili ya kuhudumia wananchi, kwa ajili ya wanaoingia na kuomba chenji.
"Hilo liliitikiwa vizuri, kwa hiyo tunaona sasa huduma ya hutoaji sarafu na noti ndogo ndogo inakwenda vizuri, hiyo ilikuwa mwaka 2019...
"Kwa hiyo tumekwenda sasa hivi karibuni baada ya kuangalia tukakuta kila tukiwauliza wenzetu (benki za biashara) mnaendeleaje na zoezi, wanasema wanaendelea vizuri, lakini ukifika kwenye maeneo unakuta watu wanasema aha! ...tunaona kama sarafu za 200 zimepungua kwenye mzunguko.
"Kwa hiyo tukafanya utafiti kuangalia kama kweli sarafu za 200, za 100 na za 50 zina uwiano gani kwenye mzunguko, kwa hiyo tukajaribu kuwasiliana na mabenki makubwa nao wakasema na sisi kama hatuzioni, sasa hamzioni zimekwenda wapi?.
"Kwanza ikumbukwe kwamba sarafu tukizitengeneza zinakaa zaidi ya miaka 30 zote bila kuharibika na zipo kwenye mzunguko, inategemea sasa na utunzaji, kwa hiyo uzipotunza vizuri si chini ya miaka 10 hadi 15 zinakuwepo.
"Kwa hiyo tulipokuja kufanya huo utafiti na kugundua wenzetu wanasema zipo kwa wananchi, sasa kwa wananchi sehemu gani, kwa hiyo utafiti mdogo tulifanya hapa Dar es Salaam tukagundua kweli watu wakichukua coins (sarafu) hawana ile shauku ya kurudisha kwenye mabenki.
"Lakini, kingine kwa nini kwenye mabenki wakati tunatoa hili tangazo letu la mwaka 2019 tuliwasisitiza huu mtindo tunatakiwa kusambaza sarafu safi kwa wananchi, na sarafu chafu tu ndiyo waruhusu kuzipokea zirudishwe kwenye Benki Kuu kama deposits kwa ajili ya kuchukua na kuzichambua.
"Zingine zilizo na kiwango zirudi kwenye mzunguko, na zingine tuziingize kwenye utaratibu wa kuziteketeza ili ziondoke kwenye mzunguko.
"Kwa hiyo ilipelekea sasa mabenki baadhi yakaweka gharama za kupokea sarafu, kwa hiyo, hiyo ikaonekana inawarudisha nyuma wananchi katika kupeleka na ku-deposits sarafu kwenye mabenki, kwa hiyo tukaliona hilo."
Amesema, Desemba, 2023,Benki Kuu iliyaelekeza mabenki yote ya biashara nchini yaanze kupokea sarafu kutoka kwa wnanachi kama desposit.
Vile vile,hata kwa wananchi ambao hawana akaunti kwenye benki hizo nao wako huru kupeleka sarafu na kubadilishiwa ili wapewe noti.
"Katika kampeni hii tumeondoa vikwazo vya upokeaji wa sarafu hizo, awali tulielekeza sarafu chafu ndio zipelekwe kwenye mabenki, lakini kwa sasa benki zimeelekezwa kupokea sarafu zote, chafu na safi.
"Lakini, hatukuishia hapo, tukaenda na kwa wananchi pia, tukasema jamani mwananchi mwenye sarafu huko azikusanye na kuzileta kwa sababu unaweza kukuta mtu amechukua ameweka kwenye kibubu, zikikaa kwenye kibubu zinaharibika.
"Kwa sababu zikikaa kwenye kibubu chenye unyevu unyevu sarafu zetu haziwezi kusahimili, kwa hiyo mwenye uwezo wa kuzitunza ni wenzetu wa mabenki na sisi wenyewe Benki Kuu.
"Kwa hiyo sasa wenzetu wa mabenki ya biashara tumeruhusu wapokee sarafu za aina zote, kwa hiyo mwanachi anaruhusiwa kwenda benki ya biashara kama ana akaunti au kama hana akaunti, au kwenda kwenye tawi la Benki Kuu ili kuweza kubadilishiwa hizo sarafu zake.
"Anazodhani hana matumizi nazo, kwa hiyo tunahamasisha hizo sarafu za shilingi 50, shilingi 100 na shilingi 200 ndizo zinazohusika kwenye mpango huo, wananchi tumewapa kipindi cha mwezi mmoja tuone kama itakuwa ni endelevu, tunaweza kuangalia kama muda unaweza kuongezwa.
"Na huu ni utaratibu wa nchi nyingi, unafanyika hivyo Kenya wana utaratibu wao wanakusanya sarafu kwa wiki, halafu zinachambuliwa zinatambulika safi, zinasambazwa tena zinarudi kwenye mzunguko kutegemea na mahitaji yaliyopo.
"Kwa hiyo na sisi tumeliona hilo, sarafu zetu mara nyingi zinakaa huko na pengine zinapotelea huko zinakuwa hazina matumizi, kwa hiyo tunahamasisha umma kutumia hii fursa ya mabenki tuliyoitoa alizo nazo na anadhani hazina matumizi, zirudi na sisi kama benki tutaziangalia na kwa utaratibu mzuri tutazichambua zinazowezakurudi kwenye mzunguko zitarudi,"amefafanua kwa kina Bw.Ilulu.