LATRA yasimamisha mabasi yote ya Kilimanjaro Express kutoa huduma, wasimamizi wawekwa mbaroni Dar

NA GODFREY NNKO 

MAMLAKA ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani imefanya ukaguzi wa kushtukiza kwa Mabasi ya masafa marefu ili kutathimini hali ya Usafiri nchini leo Januari 6, 2024.
Katika ukaguzi huo wasimamizi wawili wa kampuni ya mabasi Kilimanjaro wamewekwa mbaroni kwa kosa la kuzidhisha nauli kinyume na uliyoidhinishwa na Mamlaka pamoja na kutoa tiketi zisizo za kielekroni.

Aidha,LATRA imeyasimamisha magari yote ya Kampuni ya Kilimanjaro Express kutoa huduma ya usafirishaji kuanzia Jumatatu kutokana na kukiuka masharti ya leseni ikiwemo kutotoa tiketi ya kielektroniki na kuzidisha nauli kwa abiria.
Mkurugenzi Mkuu wa LATRA,CPA Habibu Suluo ameyasema hayo baada ya kufanya ukaguzi wa kushtukiza katika Stendi ya Kimataifa ya Mabasi ya Magufuli pamoja na ofisi za mabasi ya kampuni hiyo ya Kilimanjaro zilizopo Shekilango jijini Dar es Salaam.

Suluo amesema, mabasi hayo pekee ndio bado yanatoa tiketi zisizo za kielektroniki na kwamba yamebainika kukiuka masharti mengi ya leseni licha ya kuonywa mara kwa mara na kutozwa faini.

"Na leo tumelikamata gari jingine la kampuni hii ya Kilimanjaro inayofanya safari zake Dar es Salaam kwenda Moshi na Arusha likiwa limezidisha nauli kwa abiria, kila abiria alilipishwa nauli tofauti.

"Tukawataka wawarejeshee nauli zao, wakakubali, lakini muda mfupi tumetoka kwenye ofisi zao wakakataa tena kurejesha eti mpaka bosi wao aseme.

"Na hii siyo mara moja, wamekuwa wakifanya hivi mara nyingi na tumewaonya mara kwa mara na anaona kulipa faini ni kawaida kwake.
"Sasa sisi lengo letu ni kutaka wafuate sheria na masharti ya leseni, watoe huduma bora na siyo kutoa faini.

"Na kama anaona kulipa faini ni kawaida kwake sisi hatuwezi kuvumilia, tumetoa maagizo asitoe huduma kuanzia Jumatatu mpaka atakapofanya maboresho na kufuata masharti ya leseni yake,"amefafanua CPA Suluo.

LATRA ni mamlaka ya Serikali iliyoanzishwa kwa Sheria ya Bunge Namba 3 ya mwaka 2019.

Sheria hii ilifuta Sheria ya iliyokuwa Mamlaka ya Udhibiti wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA). 

Aidha,LATRA imepewa jukumu la kudhibiti sekta ya usafiri ardhini, hususani usafiri wa mizigo na abiria.”

Usafiri ambao unajumuisha mabasi ya njia ndefu, mabasi ya mijini, magari ya mizigo, teksi, pikipiki za magurumu mawili na matatu, usafiri wa reli na usafiri wa waya.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news