ZANZIBAR-Waziri wa Utamaduni Vijana na Michezo Zanzibar, Mheshimiwa Tabia Maulid Mwita ameupongeza Uongozi wa Klabu ya Simba kwa maamuzi ya kutangaza vivutio vya utalii katika kipindi hiki cha michuano ya Mapinduzi inayoendelea visiwani hapa.
Mheshimiwa Tabia ameyasema hayo baada ya kukabidhiwa zawadi ya jezi na Meneja Habari na Mawasiliano wa Klabu, Ahmed Ally ikiwa ni muendelezo wa kutembelea viongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ili kufahamiana na kutangaza utalii.
Waziri Tabia ameongeza kuwa, maamuzi ya kutangaza vivutio vya utalii ni mchango mkubwa wanafanya na hata kutembelea viongozi wa Serikali nalo ni jambo zuri.
“Nawapongeza sana viongozi wa Simba kwa kuliona jambo hili na kulichukulia kwa umuhimu mkubwa mmefanya jambo zuri na nawapongeza,”amesema Mheshimiwa Tabia.
Kwa upande wa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mheshimiwa Jamal Kassim Ally amesema, jambo wanalofanya linatakiwa kuigwa na timu nyingine pamoja na taasisi mbalimbali kutangaza Uualii wa nchi kwa sababu unaongeza pato la taifa moja kwa moja.
“Nawapa hongera Simba kwa kutangaza Utalii wa Zanzibar, ni maamuzi mazuri ambayo yanafaida ya moja kwa moja kwa maendeleo ya nchi,” amesema Mheshimiwa Jamal.