ZANZIBAR-Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar imesema, mazingira ya skuli yameimarika katika skuli zote za maandalizi, msingi na sekondari.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Idara ya Mipango Sera na Utafiti,Bw. Khalid Masoud Waziri wakati wa Kikao cha kuwasilisha Ripoti ya Utekelezaji wa Bajeti ya Elimu kwa kipindi cha mwezi wa Julai-Disemba,2023/2024.
Ni kwa Wajumbe wa Kamati ya Ustawi wa Jamii ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar katika Ukumbi wa Mikutano wa Wizara ya Elimu Mazizini Wilaya ya Mjini Magharibi Unguja.
Amesema, kutokana na kupungua kwa kiwango kikubwa cha msongamano wa wanafunzi darasani katika ngazi zote na baadhi ya skuli kuingia mkondo mmoja ni ishara ya kuyafikia malengo ya sekta ya elimu nchini.
Amesema, huduma za maji, vyoo, dakhalia na maabara zimeimarika katika skuli nyingi, hali ambayo inaongeza ari kwa walimu katika kufundisha kwa bidii.
Pia ameeleza kutokana na mafanikio hayo yamepelekea Zanzibar kukuza kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi wengi wa darasa la Nne, la Saba, Kidato cha Nne na Sita.
Aidha amesema, pamoja na mafanikio hayo Wizara bado inazo changamoto ya uhaba wa vifaa na wataalam katika baadhi ya skuli.
Naye Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Mhe. Lela Muhamed Mussa, ameipongeza Kamati ya Usatawi wa Jamii ya Baraza la Wawakilishi kwa kusimamia mikakati ya Serikali katika sekta ya elimu.
Amesema, katika kuelekea kwenye mageuzi ya elimu nchini, kamati hiyo inayo nafasi ya kuisaidia Wizara kuyafikia malengo hayo kwa wakati.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Ustawi wa Jamii ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Mhe. Sabiha Filfil Thani, ameitaka wizara kuvisimamia vyema Vyuo vya Mafunzo ya Amali na kuendelea kutoa hamasa kwa vijana kujiunga katika vyuo hivyo.
Mhe. Sabiha ameeleza kuwa,vyuo hivyo vitakua mtatuzi wa kero kubwa ya vijana waliokosa kuendelea na elimu ya juu.
Hata hivyo,ameisisitiza wizara kuvipatia vyuo hivyo miundombinu bora na vifaa vya uhakika ili viweze kufundisha kwa weledi zaid.
Sambamba na hayo ameitaka wizara kupitia Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu ya Zanzibar kufanya ufuatiliaji wa kiwango (asilimia) ya mkopo unaotakiwa kutolewa kwa Zanzibar.