DAR ES SALAAM-Mtendaji Mkuu wa TARURA, Mhandisi Victor Seff ameagiza kukarabatiwa haraka madaraja ya Tanganyika, Mbopo, Msumi na Goba Majengo pamoja na barabara zote zilizoharibika kutokana na mvua kubwa iliyonyesha jana jijini Dar es Salaam.
Mhandisi Seff ametoa maagizo hayo mara baada ya kufanya ukaguzi kwenye madaraja yaliyosombwa na mvua kubwa iliyonyesha tarehe 20 Januari, 2023 na kujionea uharibufu uliotokea.
Hata hivyo, Mhandisi Seff amemtaka Meneja wa TARURA Mkoa wa Dar es Salaam Mhandisi Geofrey Mkinga kuanza kazi mara moja (usiku na mchana) ili kurudisha mawasiliano ya miundombinu ya barabara zote na madaraja yaliyoharibika ili kuwezesha shughuli za kiuchumi na kijamii kuendelea kama awali.
Katika ukaguzi huo Mhandisi Seff aliweza kufanya ukaguzi wa maeneo yaliyoathirika na mvua likiwemo daraja la Tanganyika lililosombwa na maji pamoja na maingilio ya barabara ya Salasala-Benako yenye urefu wa Km. 4.6 yaliyoharibika vibaya.
Vile vile mvua hizo zimesomba daraja la Mbopo, Msumi na Goba Majengo.