*Katibu Mkuu Mahimbali asisitiza kuzingatiwa muda wa utekelezaji wake
*Awaeleza wasimamizi wa miradi mikakati kabambe ya kuendeleza Sekta ya Madini
DAR ES SALAAM-Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini,Kheri Mahimbali ameongoza kikao cha kujadili utekelezaji wa Miradi Sita (6 ) ya Uchimbaji Madini ikihusisha uchimbaji Mkubwa na wa Kati wa madini mbalimbali yakiwemo Madini Mkakati ambayo Serikali ina hisa za asilimia 16 zisizohamishika kwa kila mradi.

Kikao hicho kilichofanyika katika Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar Es Salaam Januari 26, 2024, kimelenga kupata mrejesho wa utekelezaji wa miradi hiyo, ikiwemo kufahamu changamoto na kujadili kwa pamoja namna ya kuzitatua ili kuwezesha miradi husika kutekelezwa kwa wakati kama ilivyopangwa.
Akizungumza katika kikao hicho, Katibu Mkuu Mahimbali amewaeleza wasimamizi wakazi wa miradi hiyo kuhusu matamanio ya Serikali kuona miradi hiyo ikitekelezwa kwa wakati ikiwemo matamanio ya kuanzishwa kwa migodi mingine mikubwa na ya kati kutokana na kupita kipindi kirefu cha takribani miaka16 tangu kuanzishwa kwa mgodi mkubwa hapa nchini.
Aidha, Katibu Mkuu Mahimbali ametumia fursa hiyo kuwaeleza kuhusu matamanio ya Wizara kuona watanzania wengi zaidi wakishiriki katika uchumi wa madini kupitia shughuli za usambazaji na utoaji huduma migodini.
Vilevile, Mahimbali amewaeleza kuhusu dhamira ya Serikali ya kulifanya Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kuwa shirika kubwa linalomiliki migodi mikubwa ya uchimbaji madini kwa lengo la kuwezesha manufaa zaidi ya kiuchumi kupitia rasilimali madini kwa maendeleo ya taifa.
"Tunataka baadaye STAMICO imiliki migodi iache kutoa huduma na kazi hizo zifanywe na watanzania wengine, tunataka kuwa the new South Afrika, tunataka watoahuduma kwenye migodi ya Afrika na kwingine watoke Tanzania na waingie ubia na kampuni kubwa, ninyi mnaweza kusaidia haya yote,’’amesisitiza Mahimbali.

Mbali na Katibu Mkuu na kampuni hizo, kikao hicho pia kimehudhuriwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Madini Msafiri Mbibo, Kamishna wa Madini Dkt. Abdul Rahman Mwanga, Mkurugenzi wa Biashara kutoka Tume ya Madini Andrew Mgaya na wataalam kutoka Wizara ya Madini.