NA DIRAMAKINI
KLABU ya Mlandege imeibuka mabingwa wa Mapinduzi kwa mara ya pili.
Vijana hao kutoka visiwani Zanzibar walianza kutwaa mbele ya Singida Fountain Gate mwaka 2023 na leo 2024 mbele ya Simba SC.
Ushindi huo wameupata baada Joseph Akandwanao kufunga bao kipindi cha pili akiwa ndani ya 18 akitumia makosa ya safu ya ulinzi ya Simba SC kwenye kukaba.
Mtanange huo umepigwa leo Januari 13,2024 katika Dimba la New Amani Complex jijini Zanzibar.
Tujikumbushe kidogo Simba SC ilipotokea hadi kufikia hatua ya fainali ambayo leo Mlandege imewashangaza;
Simba 3-1 JKU
Mchezo wa Simba wa kwanza katika michuano ulikuwa dhidi ya JKU uliopigwa Januari Mosi na wakaibuka na ushindi wa mabao 3-1.
Mabao yao yalifungwa na Moses Phiri na Saleh Karabaka huku moja wakijifunga wenyewe.
Simba 2-0 Singida Fountain Gate
Mechi yao ya pili ilikuwa dhidi ya Singida Fountain Gate ambayo ilipigwa Januari 5 na wakafanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-0.
Mabao yao yalifungwa na Willy Onana pamoja na Luis Miqussone.
Simba 0-0 APR
Mchezo wao wa mwisho wa hatua ya makundi ulikuwa dhidi ya APR kutoka Rwanda ambao ulimalizika kwa sare ya bila kufungana.
Walimaliza hatua ya makundi kwa kuongoza kundi wakiwa na pointi saba.
Robo fainali walicheza na Jamhuri
Katika mchuano wa robo fainali uliopigwa dhidi ya Jamhuri waliibuka na ushindi wa bao moja ambalo lilifungwa na Jean Baleke.
Nusu fainali walicheza na Singida FG
Katika mchezo wa nusu fainali walikutana na Singida Fountain Gate, Januari 8 na kuibuka na ushindi kwa mikwaju ya penati 3-2 kufuatia sare ya kufungana bao moja.
Singida walikuwa wa kwanza kupata bao moja kupitia kwa Elvis Rupia dakika ya 11 wakati wao wakisawazisha kupitia kwa Fabrice Ngoma.