Mwinjilisti Temba apokea ujumbe mzito kutoka kwa Mke wa Hayati TB Joshua, Evelyn Joshua

LAGOS/DAR-Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la Synagogue Church of All Nations (SCOAN) lililopo katika Mji wa Nigeria Lagos, Evelyn Joshua ambaye ndiye mke wa mwanzilishi wa Kanisa hilo, Nabii Mkuu Hayati TB Joshua amemwandikia ujumbe Muhubiri na Mwinjilisti wa Kimataifa, Alphonce Temba kuhusu kufungwa kuonekana kwa Channel ya Emmanuel TV kwenye King'amuzi cha DSTV.
Muhubiri na Mwinjilisti wa Kimataifa, Alphonce Temba (wa kwanza kulia) akiwa na aliyekuwa Rais wa Zambia Hayati Michael Sata wakiperuzi majarida na vitabu kutoka kwa Nabii Mkuu Hayati TB Joshua. Picha na Maktaba.

Hatua hiyo ya kufungwa kwa Channel hiyo ya Emmanuel TV inayomilikuwa na Kanisa la SCOAN chini ya Nabii Mkuu Hayati TB Joshua inakuja siku chache baada ya BBC kuibua tuhuma na kashfa za unyanyasaji wa kingono na udhalilishaji unaodaiwa kufanywa na Hayati TB Joshua kwa waumini wake waliokuwa wakitembelea kanisa lake.

Akihojiwa kwa njia ya simu kueleza juu ya ujumbe huo, Mwinjilisti wa Kimataifa Temba amebainisha kuwa, katika ujumbe huo Mke wa TB Joshua amemweleza kuwa pamoja na kufungwa kwa Channel hiyo kwenye King'amuzi cha DSTV bado itaendelea kuonekana kwenye YouTube na mitandao mingine ya kijamii.

Mwinjilisti wa Kimataifa Temba ametumia fursa hiyo kueleza namna ambavyo amekuwa karibu na familia ya TB Joshua hadi kufikia hatua ya kutumiwa ujumbe kwa njia ya email, ambapo ameelezea zaidi mahusiano ya kifamilia waliyonayo baina yao pamoja na kuweka ukweli juu ya kashfa na tuhuma hizo zilizoibuliwa na BBC hivi karibuni.

Ameeleza kwamba, yeye ndiye Matanzania wa kwanza kufahamiana na Nabii Mkuu TB Joshua, kwa sababu mara ya kwanza alimfahamu TB Joshua mwaka 2000 ambapo kipindi hicho alikuwa akiishi nchini Botswana na ndipo walipoendelea kuwa na mawasiliano. 

Kwamba mwaka 2007 Mwinjilisti Temba aliweza kumtembelea TB Joshua kwenye Kanisa lake lililopo katika Mji wa Nigeria, Lagos.

"Nilisema wazi kuwa baada ya kumtembelea TB Joshua niliweza kukaa katika Jumba lake la Kanisa lake lililopo Nigeria kwa wiki tatu, ambapo mara kwa mara tulikuwa tukikaa na kuzungumza na alivutiwa kwa kumuona Mtanzania kufika na alitamani endapo atarudi Tanzania aendelee kulitangaza Kanisa lake," amesema Mwinjilisti Temba na kuongeza,

"Alinitabiria mambo mengi na moja ya jambo ambalo alinieleza wazi ni maono aliyoyaona ndani yangu ya ukuu ya kukutana na viongozi wakubwa wa kimataifa wa ndani ya Afrika na nje ya Afrika,".

Mwinjilisti Temba anasema kuwa TB Joshua alipenda kipaji na kipawa nilichokuwa nacho, hivyo aliniomba nifanye naye kazi kwa kunipa baadhi ya bidhaa zikiwemo majarida na vitabu ili niweze kuwafikishia baadhi ya Marais barani Afrika,".
Taarifa kwa umma kutoka Kampuni ya Multchoice ikieleza kusudio la kuifunga kuonekana kwa Chennel ya Emmanuel TV kwenye King'amuzi cha DSTV

Kwamba ndipo aliweza kuondoka na vifaa hivyo ambapo kati ya Marais ambao aliwafikishia ni pamoja na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa Awamu ya Nne Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete na aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Zambia Hayati Michael Sata.

Hata hivyo Mwinjilisti Temba anasema TB Joshua alimkabidhi Bussiness kadi yake ambayo ilikuwa na namba yake ya simu maalum, ambapo tangu hapo wakawa wamawasilina mara kwa mara kwa kupigiana simu na kupeana maelekezo.

"Hivyo basi hata nilipokuwa nchini (Tanzania) niliendelea kuhusika sana kuyaeneza na kugawa baadhi ya vifaa vinavyotoka katika Kanisa lake yakiwemo mafuta ya upako, maji ya upako na ndipo kipindi hicho yalikuwa yakinenwa vibaya sana kwa sababu ya kuonekana ni maji ya Kinaigeria yenye mauza uza, lakini Muhubiri wa Kimataifa Alphonce Temba niliweza kuendelea kuongea na vyombo vya habari na waatumishi mbalimbali kwamba yalikuwa na baraka na hayakuwa na mahusiano ya mauzauza," amesema Mwinjilisti Temba na kuongeza, "Na ni kweli kabisa watu walikuwa wakifunguliwa na kuponywa magonjwa mbalimbali,".

Mwinjilisti Temba akimwelezea TB Joshua anasema ni mtumishi ambaye kumpata inaweza kuchukua miongo mingi hata zaidi ya miaka 2000 ijayo kwa sababu alikuwa na uwezo mkubwa ambao Mungu alimkirimia kiasi kwamba alikuja na mafunuo mapya ya kizazi hiki.

"Kwa mfano leo hii, maji ambayo hata Katoliki yalikuwa yakitumika, kabla hujaingia katika Kanisa Katoliki ulikuwa unayatumia, lakini pale alipoanza kuyatumia TB Joshua yalileta kelele kubwa sana hususan katika nchi yake na Bodi ya Kiroho iliyoko Nigeria ilikwenda kumkataa waziwazi na ikakata mahusiano yake kabisa pamoja na huduma zilizokuwa zikiendelea SCOAN na TB Joshua. Viongozi wote wa kiroho walimkataa hususan wa Kipentecoste walimkataa hadharani na kumkataa vibaya," anaeleza Mwinjilisti Temba.

Kwamba walimpinga na kulikuwa na makundi yaliyokuwa yakimuandika vibaya ambapo Mwinjilisti Temba ameeleza kuwa mwaka 2007 akiwa nchini Nigeria kulikuwa na magezeti na majarida mbalimbali ambayo walikuwa wakipatiwa vijana kwa ajili ya kumgawia bure kila mgeni mbaye alikuwa akiingia nchini Nigeria.

Anasema TB Joshua alikuwa anakabiliwa na vita kubwa kwani Mwinjilisti Temba anakumbuka alipatiwa jarida moja ambalo aliliangalia na kukuta likimkashfu mwanzo mwisho TB Joshua ambapo aliumia sana na kuamua kulichana ambapo lilikuwa na kurasa zaidi ya 20, kwamba lilikuwa na picha zikimuonyesha akiwa na miguu ya nyoka, lakini pia kanisa lake likionekana kuwa na nyoka wengi na mauzauza.

"Kashfa hizi zilikuwa zimetengenezwa kwa ufundi sana ili watu ambao wanakwenda Nigeria waache kwenda kwa TB Joshua na waende kwa watumishi wengine walioko nchini Nigeria. Kwahiyo vita ya dhidi ya TB Joshua ilikuwa ni kubwa sana tangu miaka hiyo. TB Joshua alihusishwa na uchawi wa baharini, alihusishwa na mauza uza mbalimbali, miujiza feki, alihusishwa na mambo mbalimbali na haya yanayosemwa sasa hivi yalikuwa ni zaidi ya hayo," amebainisha Mwinjilisti Temba.

Hata hivyo ni kwamba TB Joshua aliendelea kuwa imara, lakini ni kuwa cha ajabu pamoja na hayo TB Joshua aliwahi kualikwa Ikulu kwenda kupatiwa Nishani kutokana na shughuli mbalimbali za kijamii alizokuwa akizifanya katika jumuiya, vijiji, miji na Wilaya kwa kusaidia jamii hususan kwenye matatizo ya umeme kwani alinunua matransformer ya umeme ambapo vijiji kadhaa vilifungiwa nishati hiyo ya umeme.

Anaendelea kumwelezea TB Joshua kwa kusema kuwa alitoa misaada mbalimbali ikiwemo vyakula kwa tani za maroli kwa baadhi ya vijiji ambavyo vilikuwa na shida na alitoa bila kujali Mkoa wala Kabila pamoja na kutoa usaidizi wa Schorlaship kwa wanafunzi ndani na nje ya nchi.

Vile vile alifanya kazi kubwa ya kusuluhisha familia ya aliyekuwa Rais wa Liberia Charles Teylor ambayo ilikuwa na mzozo mkubwa na kwamba alifanya kazi kubwa kwani Marais kadhaa waliweza kuhudhuria katika Kanisa lake akiwepo aliyekuwa Rais wa Zambia Frederick Chiluba akiwa madarakani, aliyekuwa Rais wa Ghana Atta Mills, Mawaziri Wakuu na watu Mashuhuli duniani.

Hivyo kufikisha idadi ya zaidi ya watu milioni moja ambao walitembelea Kanisa lake kwa mwaka mmoja ambapo Serikali ya Nigeria iliwahi kuwatangaza kuwa miongoni mwa watu walioitembelea Nigeria kama watalii na kuliingizia Taifa mapato katika Sekta ya Utalii kwa asilimia 5 ya fedha ambazo Nigeria ilizipata katika Sekta ya Utalii.

"Hivyo kuwa baraka hata kwa Serikali na Taifa kwa ujumla, lakini pamoja na hayo yote bado alikuwa akiwa mnyenyekevu na alisafiri katika Mataifa kadha wa kadha akifanya kazi za Mahubiri na Maombezi kwani alikuwa na kipaji kikubwa cha uponyaji, zilionekana Kansa zikikauka baada ya maombezi, wako watu walioshuhudia wakiponywa magonjwa mbalimbali ikiwemo hata HIV," ameongeza mwinjilisti Temba.

Kwamba alileta amani katika familia nyingi na mambo yaote aliyoyafanya yalifanyika kwa ushuhuda kwa maana ya kwamba mtu alifika akiwa na uthibitisho wa kitaalam wa ugonjwa anaoumwa kutoka hospitali na baada ya huduma ya maombezi alikuja tena kutoa ushuhuda wa namna alivyopona ugonjwa wake.

"Hakika katika suala la maombezi, uponyaji, karama aliyokuwa nayo ni kubwa na ndipo hapo kelele nyingi zilipoanza kuisha na aliendelea kuboresha jiji la Lagos kwa kupokea idadi kubwa sana ya wageni kwani katika historia ya Nigeria hakuwepo Mtumishi wa Kiroho aliyepokea washirika na wageni mbalimbali kutoka kila pembe ya Dunia kama alivyokuwa Nabii Mkuu TB Joshua. Hakika alikuwa ni mtu mkuu," amesema Mwinjilisti Temba na kubainisha,

"Hivyo basi mimi nilikuwa ni miongoni mwa Ma-Patner wa Emmanuel TV nikiwa na namba yangu ya U-Patner TZ 003698. Kwa hiyo hiyo ndiyo namba yangu ya U-Patner ndiyo maana habari zote zilizokuwa zikifanyika na zilizotokea katika Kanisa la Synagogue SCOAN na nilikuwa sehemu ya kujulishwa kama Patner wa kanisa hilo. Kama Patner wa TB Joshua, na kama mtu wake wa karibu ikizingatiwa nilitumwa kwa viongozi na niliwasilisha na ndipo hapo basi urafiki wangu na Nabii Mkuu TB Joshua ulikwua karibu," ameeleza Mwinjilisti Temba.

Mwinjilista Temba ameeleza kuwa jambo ambalo analikumbuka ambalo alilifanya Tanzania, ni kumshawishi kuja na kuwa sehemu ya ujio wake nchini Tanzania na kwamba siku moja kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2010 akiwa na TB Joshua majira ya saa 6 usiku walifanya conference call kwa kupigiana simu ambapo waliongea pamoja na Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete ambaye alikuwa akigombea Muhula wa pili.

Hivyo TB Joshua aliwaongoza kwenye Conference call kwa kufanya maomba kwa saa nzima pamoja na kutoa utabiri ambao alikuwa akimtabiria Rais Kikwete juu ya nini ambacho kingetokea katika uchaguzi huo ambapo ilitokea kama alivyotabiri jambo ambalo lilimshangaza Dkt. Kikwete na asubuhi yake kabla ya uchaguzi waliwasiliana jambo ambalo lilimfurahisha.

Kwamba ilifika wakati TB Joshua alimuelekeza Mwinjilisti Temba kupeleka Dishi lake Ikulu ili Rais Dkt. Kikwete aweze kumuona lakini Rais Kikwete alikataa kwamba kwa ajili ya usalama na protocal za Ikulu hakuna kitu kilichopo nje ya mfumo kinachoweza kupelekwa na kutumika ndani ya Ikulu.

Mwinjilisti Temba anasema kwa ukaribu huo, jambo lingine analolikumbuka ni 2011 baada ya uchaguzi wa Zambia ambapo Rais Michael Sata alishinda, walifanya pia Conferenc Call kati yao watatu yaani Mwinjilisti Temba, Michael Sata na TB Joshua, hata hivyo Mwinjilisti Temba anasema kabla TB Joshua hajaongea na Sata alimwambia Sata kwamba Mwinjilisti Temba angekuwa msaada mkubwa katika kumshauri na Serikali yake hivyo awe karibu naye.

"Na ndiye aliyemshauri niwe mshauri wake na niwe karibu yake ili niweze kumshauri katika Serikali yake na nilifanya kazi hiyo kwa miaka 3," anasema Mwinjilisti Temba.

Kwamba TB Joshua alikuwa amemweleza kuwa kabla ya kuongea na Sata alikuwa na umuhimu mkubwa wa yeye TB Joshua kufika Ikulu ya Zambia kwa sababu alikuwa bado anaona unabii wa kifo kitakachoendelea kutokea Ikulu kwani Ikulu hiyo ilikuwa bado inaonyesha yeyote atakayeendelea kukaa pale atakutwa na mauti.

Hivyo Mwinjilisti Temba anaeleza kuwa baadaye alimweleza Rais Sata juu ya jambo hilo, lakini kwa kuwa aliona tayari yuko naye alimjibu kwamba watapanga ili waweze kumpokea TB Joshua, lakini kadri siku zilivyozidi kwenda hakushughulikia jambo hilo hata pale alipomkumbusha na kumsisitiza mara kwa mara aliendelea kuwa kimya na hati maye Rais Sata alifariki akiwa Ikulu.

Kwamba baada ya kifo cha Rais Sata, Mwinjilisti Temba anasema aliendelea kumheshimu na kumuogopa sana Nabii Mkuu TB Joshua. Hivyo Mwinjilisti Temba anasema yeye ndiye anayemfahamu TB Joshua kwa sababu ya yale manane aliyomwambia kwamba pale Ikulu ya Zambia inashida kubwa na kwamba anaona mauti yakiendelea kuwakumba Marais watakaokuwa wakiishi katika Ikulu hiyo kama ilivyotokea kwa Levy Mwanawasa ambaye naye alifariki akiwa Ikulu baada ya kushinda Urais katika uchaguzi wa 2006.

Kwamba hata alivyokwenda hivi karibuni kuonana na Rais wa Zambia wa hivi sasa Haikande Hechilema aliendelea kulisisitiza jambo hilo kwa msaidizi wake na Mwenyekiti wa Chama chake, lakini cha kushangaza Tangu Rais huyo aapishwe hajawahi kuishi katika Ikulu ya Zambia na anaishi nyumbani kwake.

Hata hivyo Mwinjilisti Temba anasema kuwa haijulikani ni sababu gani Rais huyo haishi katika Ikulu ya Zambia, lakini inadaiwa huenda ni kutokana na Maono ya TB Joshua ya kwamba mauti yataendelea kuwakuta wote watakaoishi katika Ikulu hiyo kwani haipo salama.

Mwinjilisti Temba akizungumzia kuhusu sababu za kuibuka kwa kashfa na tuhuma shidi ya TB Joshua, anasema kuwa ni kutokana na uzushi uliotengenezwa na Mzungu aliyekuwa akimsaidia TB Joshua katika kuandaa mikutano mbalimbali katika mataifa mbalimbali na ni baada ya kuwa miongoni mwa watumishi wasaidizi walioondolewa kwenye nafasi zao baada ya Bodi ya Kanisa Kumthibitisha Mke wa TB Joshua, Evelyn kuwa Mchungaji Kiongozi wa SCOAN jambo ambalo hakukubaliana nalo.

Hivyo Mwinjilisti Temba amewataka Watanzania kutokuingia katika uchonganishi huo na kuwataka kumshukuru TB Joshua kwa mchango wake kwa amani na utulivu wa Tanzania baada ya Uchaguzi wa Mwaka 2015 ambapo alikuja nchini Tanzania na kufanya mazungumzo Ikulu na aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano Dkt. John Pombe Magufuli na baada ya hapo alikwenda Masaki kufanya mazungumzo na Edwad Lowasa pamoja na ujumbe wa Chadema akiwemo Freeman Mbowe.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news