Mwinjilisti Temba atemewa mate ya baraka na bibi, afunguka mazito

KILIMANJARO-Zikiwa zimepita siku zaidi ya 20 tangu Nabii wa Kimataifa kutoka Kingdom Embassy Church nchini Marekani, Passion Java kumtabiria Mwinjilisti wa Kimataifa, Alphonce Temba kuwa, anaona baraka kubwa katika maisha yake, kwa mara nyingine tena ametemewa mate ya baraka na bibi wa miaka 90.
Desemba 8, 2023 katika Usiku wa Maajabu ulioandaliwa na Mtumishi wa Mungu, Nabii Clear Malisa jijini Dar es Salaam na kuwakutanisha maelfu ya watu, Nabii Java alimuinua Mwinjilisti Temba katika kusanyiko hilo na kumweleza kile ambacho Mungu amekusudia kwenda kukifanya katika maisha yake.

“…ninaweza kutabiri, mimi sikujui baba, lakini kuna baraka juu ya maisha yako, ninaona miguu miwili, mguu mmoja ninaona kwenye huduma, mguu mwingine ninaona kwenye siasa.

“Unafanya huduma? Ndiyo...una uhakika? …ndiyo. Unafanya siasa…ndiyo, sikujui wewe, lakini Mungu anakujua wewe, ninasikia kitu kama Alphonce…Alphonce …(ni mimi) Mungu ameniambia nimguse Alphonce leo na nitaachilia baraka mara mbili.

“Baraka kwa ajili ya uongozi (siasa) na baraka kwa ajili ya huduma. Ninakuangalia, simuoni mke…ni kweli, Mungu anasema atamrejesha na atauponya moyo wako, na ninakugusa kutakuwa kuna baraka juu yako ambayo itagusa maisha ya watu wengi na kupanua himaya yako,”Nabii Java kutoka nchini Marekani alimtabiria Mwinjilisti Temba.

Baada ya utabiri huo, Mwinjilisti Temba leo Januari 4, 2024 akiwa kijijini kwao huko Kiruwa Vunjo Kokira Kwamare katika Halmashauri ya Wilaya ya Moshi Vijijini mkoani Kilimanjaro, bibi yake wa miaka 90 amemtemea mate ya baraka na kumtamkia kuwa, atastawi kila akanyagapo iwe Mashariki, Kusini, Magharibi na Kaskazini.
Aidha, bibi huyo amemwambia Mwinjilisti Temba kuwa, pale Mungu anapokwenda kumpa nafasi kubwa zaidi maishani mwake aendelee na moyo wake wa siku zote wa kuendelea kusikiliza, kushauri na kujitolea kwa ajili ya kugusa maisha ya wengine kupitia mahitaji mbalimbali.

"Ninakuona wewe ni kiongozi mkubwa sana ajaye nchini, Mungu akatimize hilo kwako, lakini mjukuu wangu ukifanikiwa endelea kuwa baraka kwa jamii na Watanzania wote bila kujali kabila, dini, rangi au umbile la mtu, Mungu akubariki sana,"Bibi huyo amemtabiria Mwinjilisti Temba huku akimtemea mate ya baraka.

Mwinjilisti Temba ambaye kama kawaida yake pia leo amegusa maisha ya wazee hao kwa kuwapatia fedha, mahitaji muhimu na jora za kanga kwa ajili ya bibi amesema kuwa, tangu mwaka 2010 amekuwa na utaratibu wa kuwabariki wazee mbalimbali kadri Mungu anavyomjalia.

Amekuwa, akigawa fedha taslimu shilingi 20,000 kwa kila kaya katika ukoo ambapo kuna wazee wa kuzidi miaka 70 kwa ajili ya kupata fedha za kupima afya zao na kuchukua vipimo.

Mwinjisti Temba ameamuwa kuyaweka wazi maisha yake kwa sababu mara baada ya mwaka 2010 kuzungukia wazee katika ukoo na kuwapa fedha za vipimo hakuwa na uwezo mkubwa wa kifedha kwani,aliishi katika nyumba ya kupanga Temboni na kulipa kodi kwa shida sana.

Aidha,baada ya tendo hilo la kuwabariki wazee alivyorudi Dar es Salaam ghafla Mungu alifungua milango na kupata maono ya kufungua Radio ambayo pamoja na kutokuwa na uwezo wa kuwa na milioni 400 Mungu akafanya miujiza.

Ndipo akaifungua redio bila mchango wa mtu yeyote kwa miujiza mikuu ya Mungu iitwayo Penuel 105.1 Fm iliyoko Moshi mkoani Kilimanjaro.

Vile vile, akiwa kijijini hapo, Mwinjilisti Temba alitoa wito na kutoa siri iliyoko katika kanisa leo nchini na mataifa mengine mbalimbali duniani.

“Kwa uzoefu wangu wa miaka 24 katika huduma nimejifunza vitu viwili ambavyo nilivifanyia utafiti mkubwa sana,kwanza nilijifunza juu ya kwa nini kumekuwa na umaskini mkubwa sana ndani ya kanisa na kuwageuza watu au watu kugeuka kuwa wa kuomba sana makanisani na kutoa sana makanisani matokeo yake wanaendelea kuwa kwenye umaskini mkubwa.

“Umaskini ambao umechangia wengi familia zao kuharibika, kuacha kazi au kuendelea kuwa katika hali ngumu za kimaisha na wengine kuendelea kuacha imani na kudumbukia kwenye wimbi la ulevi au kutotamani kabisa kusikia mambo ya watumishi pamoja na ibada.

“Jambo la pili ni tatizo la ndoa ambalo kila kukicha leo ndoa zimekuwa zikivunjika si kwa watumishi na washirika wamekuwa wakiachana na kuachana huko kumepelekea kutokuwa na nidhamu, kwani baadhi ya ndoa hizo zinazovunjika zinaishia katika mitandao kwa watumishi wa Mungu kuendelea kuchambana.

“Kutoleana siri za ndani, jambo ambalo limeendelea kuwashusha moyo sana baadhi ya watumishi hususani wachanga wa imani na kuwavunja moyo kwa sababu ya kukosekana kwa shuhuda ya ndoa ambazo zilikuwa zikipendwa na kutarajiwa na wengi, nyingine zilikuwa zimeingia katika uaminifu na ushuhuda mkuu sana hata miongoni mwa watumishi,”amefafanua Mwinjilisti Temba.

Aidha, baada ya kugundua kinachotesa na nini shida na kwa nini watu wengi wamekuwa wanakesha makanisani kupita maelezo, na je, msingi wa kumtafuta Mungu ni msingi wa kibinafsi zaidi kama tunavyoona watu wengi ambao wamekuwa na maombi ya muda mrefu, lakini ukiangalia maisha yao wamedumbukia kwenye umaskini mkubwa, anasema aligundua yako baadhi ya mambo hayajajengewa msingi.

“Ama hayafundishwi, ama washirika ambao wamekwisha komaa hawayafuatilii kwa sababu wameshayajua maandiko, na leo hii Biblia imekuwa kila mahali hata kwenye simu, kwenye vitabu mbalimbali yanaelezea, maandiko yamekuwa mengi kwenye vitabu vya watumishi wa Mungu, lakini bado,”

Mwinjilisti Temba amefafanua kuwa, makanisa kadhaa yamezipa majina laana na kuwaambia washirika wao wanalaana za familia,aridhi, matambiko ya muzimu ya ukoo na madhabau za majina yao, kabila zao na kadhalika.

"Kumbe wangeliuliza mahusiano yao na wazazi wangejua kumbe toka baba au mama zao hawakuwaheshimu wazazi wao ndiyo maana wanateseka sana ukisoma neno la Mungu katika Ezekiel 16.44.
"Tazama, kila mtu atumiaye mithali atatumia mithali hii kinyume chako, akisema, kama mama ya mtu alivyo, ndivyo alivyo binti yake.

Amesema, neno la Mungu katika kitabu cha Kutoka 20.12 linasema, Waheshimu baba yako na mama yako; siku zako zipate kuwa nyingi katika nchi upewayo na Bwana, Mungu wako.

Pia, amesema Mathayo 15.4 inasema, Mungu alisema, Mheshimu baba yako na mama yako, na amtukanaye baba yake au mama yake kufa na afe.

"Sasa mama alikuwa na uovu wa kutokutii na mtoto atii kisha mchungaji amuombee eti afanikiwe hilo halipo, rudini mkatii na kuwaheshimu wazazi, kuwanunulia vitu na kuwapa pesa hata kama unamtunza fanya zaidi ya hapo.

"Wako ambao baada ya kuokoka au kuoa unaambiwa na mkeo eti mama yako ni mchawi usimpe kitu atawaloga, bibi yako ni mchawi eti atawaloga, lakini amuambiwi alishindwaje kukuloga tangu tumboni hadi umemaliza masomo, kumbe wewe ndiye umeoa mchawi au mtu asiye na uelewa wa baraka.

"Kama kweli uchawi upo pitisha kwa Mchungaji wako aombee hizo nguo mpelekee mzazi au mchungaji hana hupako wa kuombea? Tafakari njia zako sana wapi unakwama,"amesisitiza Mwinjilisti Temba.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news