NECTA yafuta na kuzuia matokeo ya mamia ya watahiniwa Kidato cha Nne 2023

NA DIRAMAKINI

BARAZA la Mitihani Tanzania (NECTA) limefuta matokeo yote ya watahiniwa 102 wa Maarifa na 101 wa mtihani wa Kidato cha Nne ambao wamebainika kufanya udanganyifu katika mtihani.
Hayo yameelezwa leo Januari 25,2024 na Katibu Mtendaji wa NECTA, Dkt. Said Ally Mohamed wakati akitangaza matokeo hayo jijini Dar es Salaam.

Matokeo hayo yanatokana na mtihani wa kidato cha nne uliofanyika Novemba 2023 nchini.

“NECTA imefuta pia matokeo ya watahiniwa watano wa kidato cha nne walioandika lugha ya matusi katika skripti zao.

"Matokeo hayo yamefutwa kwa mujibu wa Kifungu cha 5 (2) (j) cha sheria ya Baraza la Mitihani sura ya 107 kikisomwa pamoja na Kifungu cha 30(2) (b) cha Kanuni za Mitihani Mwaka 2016.

“NECTA imezuia pia kutoa matokeo ya Watahiniwa 376 ambao walipata matatizo ya kiafya na kushindwa kufanya mtihani wa kidato cha nne mwaka 2023 kwa masomo yote au idadi kubwa ya masomo.

"Watahiniwa husika wamepewa fursa ya kufanya mtihani kwa masomo ambayo hawakuyafanya kwa sababu ya ugonjwa mwaka 2024 kwa mujibu wa Kifungu cha 32(1) cha Kanuni za Mitihani,”amesema Dkt.Mohamed.

Amesema, katika mtihani huo jumla ya watahiniwa 484,823 sawa na asilimia 87.65 ya watahiniwa waliofanya mtihani wamefaulu.
“Wasichana waliofaulu ni 257,892 sawa na asilimia 86.17 wakati wavulana waliofaulu ni 226,931 sawa na asilimia 89.40, mwaka 2022.

"Watahiniwa waliofaulu walikuwa ni 476,450 sawa na asilimia 86.78, hivyo ufaulu wa watahiniwa umeongezeka kwa asilimia 0.87 ikilinganishwa na mwaka 2022.

"Kati ya wanafunzi hao waliofaulu kuna watahiniwa wa shule na watahiniwa wa kujitegemea ambapo jumla ya watahiniwa wa shule 471,427 kati ya 527,576 wenye matokeo ambao ni sawa na asilimia 89.36 wamefaulu ambapo wamepata madaraja ya I, II, III na IV.

"Mwaka 2022 watahiniwa waliofaulu walikuwa 456,975 sawa na asilimia 87.79, hivyo ufaulu umeongezeka kwa asilimia 1.57.

“Watahiniwa wa kujitegemea waliofaulu mtihani ni 13,396 sawa na asilimia 52.44, mwaka 2022 watahiniwa wa kujitegemea 19,475 sawa na asilimia 68.34 walifaulu mtihani huo, hivyo ufaulu wa watahiniwa hao wa kujitegemea umeshuka kwa asilimia 15.90 ukilinganisha na mwaka 2022,”amesema Katibu Mtendaji huyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

1 Comments

  1. Baraza la mitihani napenda kutoa ombi ya shule ya secondary Tunduma Tc ifuatiliwe zaidi kuanzia sector za uongozi wa juu hadi za chini maana ni kama kuna mambo yasiyo kuwa ya haki katika shule hiyo

    ReplyDelete
Previous Post Next Post

International news