NHC, wabia waanza safari ya kihistoria nchini

NA GODFREY NNKO

SHIRIKA la Nyumba la Taifa (NHC) limesaini mikataba ya ubia na wabia kwa ajili ya kuendeleza miradi 21 iliyoidhinishwa.
Miradi hiyo ina thamani ya zaidi ya shilingi Bilioni 271 ikilinganishwa na thamani ya sasa ya majengo hayo ambayo ni shilingi bilioni 59.

Hayo yameelezwa leo Januari 29,2024 na Mkurugenzi Mkuu wa NHC,Hamad Abdallah wakati akizungumza mbele ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,Mheshimiwa Jerry Silaa.

Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mheshimiwa Jerry Silaa amewapongeza wote walioshiriki kubuni wazo la kuihuisha Sera ya Ubia mwaka 2022 ambayo leo Watanzania wameshuhudia utiaji saini wa utekelezaji wa sera hiyo.
"Juhudi za shirika letu la nyumba za kuwa wakereketwa wa maendeleo katika sekta ya nyumba ndiyo imetufanya tujumuike hapa leo kushuhudia mabadiliko haya makubwa. Hakika hili ni jambo jema.

"Serikali inafahamu kuwa mlishawaalika wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuomba uendelezaji wa maeneo ya shirika yaliyopo katikati ya miji yetu.

"Aidha, serikali iliwaagiza mhakikishe mnakuwa makini katika kuwachuja wabia hawa ili hatimaye tuwapate waendelezaji makini na wenye uwezo wa kukamilisha miradi kwa wakati.
"Ni imani yangu kuwa maelekezo hayo yamezingatiwa vyema na hivyo leo kutufanya kushuhudia kundi la kwanza la wabia wanaoanza kutekeleza miradi itakayoongeza ufanisi kwa shirika na nchi yetu. Nawapongeza sana kwa hilo."

Amesema, Serikali ilielekeza kuwapo umakini wa kuchuja waombaji wa miradi ya ubia kutokana na changamoto zilizojitokeza huko nyuma wakati wa utekelezaji wa miradi ya ubia.

Waziri amesema,Sera ya Ubia ya kwanza ya Shirika iliyopitishwa mwaka 1993 na kufanyiwa marekebisho kadhaa katika miaka ya 1998, 2006 na 2012 ilikuwa na changamoto mbalimbali kutokuwa na uwiano wa umiliki wa hisa za mradi, kutokuwa na kigezo cha thamani ya uwekezaji kwenye mradi ukilinganisha na thamani ya kiwanja cha shirika ili kuwa na miradi inayoendana na uwekezaji wa eneo husika.
Sambamba na kuwapa wabia miradi zaidi ya mmoja hali iliyowafanya miradi kutokamilika.

Aidha, amesema sera hiyo haikuwa na vigezo vya kufanyiwa upekuzi wa kina (due diligence) kwa makampuni yanayoomba miradi ya ubia ili kujiridhisha na uwezo wao wa kutekeleza miradi na iliruhusu baadhi ya wabia kutumia hati ya kiwanja cha shirika kama dhamana katika kupata mtaji wa kuwekeza kwenye mradi wa ubia.

Amesema, changamoto hizo zote zilizochangia miradi ya ubia kutokamilika kwa wakati sasa zimeondolewa katika sera hii mpya ya ubia iliyoboreshwa.
"Hivyo, hatutarajii kuona hata mradi mmoja unasusua na tunatarajia miradi yote ikamilike kwa mujibu wa mikataba husika.

"Miradi inayotarajiwa kutekelezwa itaongeza idadi ya nyumba za kuishi pamoja na maeneo ya biashara na hivyo kuchangia kutatua changamoto ya makazi bora na maeneo bora ya kibiashara."

Amesema, utekelezaji wa sera ya ubia ni utekelezaji wa maono ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuongeza ushirikishwaji wa sekta binafsi.

Pia, huu ni utekelezaji wa maelekezo ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020 inayoelekeza kuongeza upatikanaji wa nyumba bora.
Mkurugenzi Mkuu wa NHC amesema, Sera ya ubia inalenga kujenga mazingira bora ya kibiashara, kuvutia uwekezaji na kuimarisha ushirikiano kati ya serikali, sekta binafsi na jamii kwa ujumla.

Katika hafla hiyo ambayo imefanyika Ukumbi wa Kambarage House jijini Dar es Salaam, pia imewakutanisha pamoja viongozi wa jiji la Dar es Saalam,wabia, Menejimenti na wafanyakazi wa NHC.

Mkurugenzi Mkuu wa NHC amesema, sera ya ubia ya NHC ilianza kutekelezwa kuanzia mwaka 1993.

Aidha,sera hiyo imekuwa ikifanyiwa maboresho mara kwa mara na maboresho ya mwisho yalifanyika 2022.
"Maboresho hayo yalilenga kuondoa changamoto kadhaa ambazo zilikwamisha utekelezaji wa miradi hii ya ubia kwa ufanisi.

"Mheshimiwa, kutokana na wito wa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan wa kuyataka mashirika na taasisi mbalimbali za umma kushirikiana na sekta binafsi katika kutekeleza miradi ya maendeleo.

"Shirika la Nyumba la Taifa lilifanya maboresho makubwa ya sera yake ya ubia. Maboresho hayo yalilenga kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa miradi ya ubia na kuongeza tija zaidi kwa Shirika, wawekezaji na Taifa kwa ujumla,"amefafanua Abdallah.

Vile vile, Mkurugenzi Mkuu amesema, maboresho yaliyofanyika yaligusa maeneo kadhaa ikiwemo kurekebisha uwiano wa umiliki wa hisa za mradi.
Ni kutoka hisa za mwisho za shirika za asilimia 50 (baada ya miaka 12) kuwa hisa za mwisho za shirika za asilimia 60 (baada ya miaka 15) mpaka asilimia 75 (baada ya miaka 25).

Pia,kuweka kigezo cha thamani ya uwekezaji kwenye mradi wa mara nne ya thamani ya kiwanja cha shirika, ili kuwa na miradi inayoendana na uwekezaji wa eneo husika.

Abdallah amesema,nyingine ni kuzuia utoaji wa miradi zaidi ya mmoja kwa mwekezaji mmoja ili kuwawezesha kutekeleza mradi mmoja mpaka ukamilike kabla ya kuomba mradi mwingine.

Nyingine ni kuweka vigezo vya kufanyiwa upekuzi wa kina (due diligence) kwa makampuni yanayoomba miradi ya ubia ili kujiridhisha na uwezo wao wa kutekeleza miradi.
Aidha, kuzuia hati ya kiwanja cha shirika kutumika kama dhamana katika kupata mtaji wa kuwekeza kwenye mradi wa ubia.

Mkurugenzi Mkuu huyo amesema kuwa, baada ya uzinduzi wa sera hiyo ya ubia ya Shirika la Nyumba la Taifa, uliofanywa na Mhe. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa (Mb.) Novemba 16, 2022, shirika lilitangaza orodha ya viwanja 87 vilivyopo katika mikoa 18 kwa ajili ya uwekezaji.

Amesema,viwanja 34 ambavyo ni sawa na asilimia 39 ya viwanja vyote vilivyotangazwa vipo katika Mkoa wa Dar es Salaam.

"Mheshimiwa Waziri, baada ya kutangaza maeneo hayo ya uendelezaji tulipokea jumla ya maombi 59 ya kuendeleza viwanja 28 na kuchambuliwa kwa kuzingatia vigezo tisa vilivyowekwa.

"Vigezo hivyo ni barua ya maombi, andiko la mradi, dhana ya mradi, gharama ya mradi, wasifu wa kampuni, nyaraka za usajili wa kampuni, uwezo wa kifedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi.
"Nyingine ni taarifa za kifedha zilizokaguliwa pamoja na ujuzi na uzoefu wa kampuni katika utekelezaji wa miradi ya uendelezaji milki kuu,"amesema.

Amebainisha kuwa, baada ya uchambuzi na tathmini ya kina, jumla ya waleta maombi 24 walipendekezwa kwa ajili ya kuidhinishwa na Menejimenti na Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika.

Bodi iliidhinisha maombi hayo 24 na baada ya kuendelea kuchambua kwa kupitia vigezo vyote muhimu, miradi mitatu imeondolewa kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo wabia kushindwa kuendelea na nia yao ya kuendelea na utekelezaji wa miradi.

"Ili kuwa na mikataba yenye tija shirika na wawekezaji, Mwanasheria Mkuu wa Serikali alihusishwa katika kuihakiki na kuidhinisha mikataba yote ya waliofanikiwa kupata miradi.
"Mheshimiwa Waziri, miradi 21 iliyopitishwa inajumuisha viwanja 16 vilivyopo Kariakoo, kiwanja kimoja kilichopo Upanga, viwanja 2 vilivyopo jijini Mwanza na mradi mmoja kwa kiwanja kilichopo Iringa.

"Miradi yote hii 21 iliyoidhinishwa ina thamani ya jumla ya takribani shilingi Bilioni 271 ikilinganishwa na thamani ya sasa ya majengo hayo ambayo ni shilingi Bilioni 59."

Amesema, miradi inayotarajiwa kutekelezwa itaongeza idadi ya nyumba za kuishi pamoja na maeneo ya biashara na hivyo kuchangia kutatua changamoto ya makazi bora na maeneo bora ya kibiashara.

"Kwa mfano, kwa miradi inayotarajiwa kutekelezwa eneo la Kariakoo itakuwa na jumla ya wapangaji 2,011 (maduka 1,258 stoo 500 na nyumba za makazi 253 ikilinganishwa na idadi ya sasa ambayo ni wapangaji 190 (maduka 118 na nyumba za makazi 72)."
Mkurugenzi Mkuu huo amesema, utekelezaji wa miradi hii inatarajiwa kuanza kuanzia mwezi Februari 2024 kila mradi unapopata kibali cha ujenzi kutoka mamlaka husika.

Miradi yote inatarajiwa kuchukua muda wa miaka 2-3 kukamilika kulingana na ukubwa wa kila mradi.

Abdallah amesema,kabla ya kuanza utekelezaji wa miradi hii iliyokuwa imeombwa na kuidhinishwa na bodi, shirika lilitoa notisi ya miezi mitatu, ingawa matakwa ya kisheria notisi ni ya mwezi mmoja.

"Hata hivyo, kwa kuzingatia maombi ya wapangaji na kwa maelekezo ya wizara yetu ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, shirika liliongeza muda wa miezi mingine minne na hivyo notisi za kupisha ujenzi kuwa za miezi saba.
"Hivyo, wapangaji walipatiwa notisi zilizoishia Desemba 31,2023. Aidha, katika vikao vyetu vya mara kwa mara na Kamati ya Wapangaji wa eneo la Kariakoo, ilikubalika kuwa kutokana na mchakato mrefu wa upatikanaji wa vibali vya ujenzi, shirika litakuwa linaongeza mwezi mmoja kwa miradi ambayo inakuwa haijapata vibali vya ujenzi.

"Notisi ya mwisho tuliyowapa wapangaji inaishia Januari 31, 2024. Tunaishukuru Kamati ya Wapangaji wa eneo la Kariakoo na wapangaji wote waliokubali kupisha ujenzi kwa maslahi ya Taifa letu.

"Hawa wameingia katika historia ya nchi yetu ya kuboresha miji yetu, hususan eneo nyeti la biashara za kimataifa la Kariakoo,"amefafanua Mkurugenzi Mkuu wa NHC.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news