NHC yamuondoa kwa nguvu mvamizi aliyekataa kuachia nyumba Kilimanjaro

NA DIRAMAKINI

SHIRIKA la Nyumba la Taifa (NHC) limemuondoa kwa nguvu, Dani Paul Kihauka aliyekaidi agizo la kutakiwa kuachia nyumba ambayo kisheria ni mali ya shirika hilo mkoani Kilimanjaro.
Hayo yamebainishwa Januari 8,2023 na Meneja wa Habari na Mawasiliano NHC, Muungano Saguya wakati akizungumza na wanahabari mjini Moshi.

Saguya amesema, nyumba hiyo ilitaifishwa na Serikali kupitia Sheria Na. 13 ya mwaka 1971, ambapo ilitwaliwa na kuweza kumilikiwa na Serikali.

“Kazi ambayo tumeifanya hapa mjini Moshi (Mkoa wa Kilimanjaro) ni kazi ya Nyumba Na.17 na Na.18 Kitalu K Barabara ya Market hapa mjiini Moshi.

"Hii ni moja ya nyumba ambayo ilitaifishwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Sheria Na.13 ya mwaka 1971, nyumba hii ni moja ya nyumba zilizotwaliwa na kuweza kumiliwa na Serikali kupitia iliyokuwa Msajili wa Majumba Tanzania.

“Lakini, baadaye baada ya kuunganishwa iliyokuwa Msajili wa Majumba na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) ambayo NHC nayo ilianzishwa kwa Sheria Na.45 ya mwaka 1962, nyumba zote zilizokuwa chini ya Msajili wa Majumba zilirejeshwa katika Shirika la Nyumba la Taifa.

“Na ikiwa ni moja ya nyumba hii tunayozungumza leo, sasa mmiliki wa wa mwanzo wa nyumba hii alikuwa anaitwa Bw.Paul Kihauka Njau na huyu Bw.Paul Kihauka Njau ambaye alikuwa mmiliki wa nyumba hii kwa mujibu wa utaratibu uliokuwepo kipindi kile, Serikali ilikuwa inachukua nyumba, lakini inamuachia mmiliki wa awali sehemu ya nyumba.

“Kwa hiyo huyu bwana (Njau) aliachiwa apartments mbili zilizopo juu ya jengo hilo, lakini apartments zingine zote zilikuwa zinapaswa kuwa chini ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yaani ziwe chini ya Msajili wa Majumba.

“Na nyumba hizi,umiliki wa sehemu hizi ambazo alikuwa anapewa na Serikali ulikuwa unakoma pale mtu anapofariki dunia.

“Yaani unapewa sehemu unaitumia, lakini ukifariki dunia umiliki wake unarejea serikalini, kwa maana alipaswa alipofariki tarehe 17 Februari 2002, huyu Bw.Paul Kihauka Njau nyumba hiyo familia yake wairejeshe serikalini kwa maana wairejeshe Shirika la Nyumba la Taifa.

“Sasa, Shirika la Nyumba la Taifa katika mazoezi yanayoendelea ya kuhakiki nyumba zake,na kujiridhisha nani anayekaa kwenye nyumba hizo ilikuja kubaini kwamba mmiliki wa awali, Bw.Paul Kihauka Njau alishafariki na nyumba hiyo ambayo tunaizungumzia leo ikawa inaendelea kutumika na kijana wake.

“Sasa, baada ya kubaini hilo Shirika la Nyumba la Taifa liligundua kwamba, apartment namba 006 katika nyumba hiyo inakaliwa kinyemela na Bw.Dani Paul Kihauka ambaye ni mtoto wa marehemu.

“Shirika lilifanya juhudi za mara kwa mara za kumuita mtoto huyo wa marehemu ili hatimaye aweze kuelimishwa juu ya sheria iliyopo, lakini pia kama angehitaji upangaji aweze kupatiwa upangaji.

“Lakini,mwisho hakuweza kukubali na hakuweza kuja kuongea na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Mkoa wa Kilimanjaro, hivyo ikabidi NHC Mkoa wa Kilimanjaro ichukue hatua thabiti za kurejesha nyumba hiyo ya Serikali mikononi mwa shirika.

"Ndipo tarehe 29 Desemba, 2023 kwa kutumia dalali wa Mahakama wa Majembe Auction Mart shirika liliweza kufanya zoezi la kuweza kumuondoa mvamizi huyo kwenye nyumba hiyo.

“Lakini, katika hali ya kushangaza Bw,Dani Kihauka aliwapiga wafanyakazi wa Majembe Auction Mart ambao walikuwa wakitekeleza wajibu wao wa kisheria,waliokuwa wamepewa na Shirika la Nyumba la Taifa kwa mujibu wa Sheria Na.11 ya mwaka 2005.

"Baada ya kufanya hivyo, shirika liliweza kufanya juhudi mbalimbali ikiwemo kumuita na kuvielekeza vyombo vya Serikali ili viweze kuchukua hatua za huyo mtu ambaye inafika mahali anapiga watu kwa mali za Serikali.

“Sasa, niseme tu leo nimewaita hapa,kwa sababu leo tarehe 8 Januari, 2024 Shirika la Nyumba la Taifa likimtumia dalali wa Mahakama, Majembe Auction Mart limeweza kumtoa Bw.Dani Kihauka katika apartment hiyo ambayo anaitumia kinyemela kama mvamizi na apartment hiyo sasa Shirika la Nyumba la Taifa linaenda kuipanga kwa Mtanzania yeyote ambaye atakuwa anahitaji.

"Sasa, nitoe wito tu katika Shirika la Nyumba la Taifa ambalo lina nyumba zaidi ya 18,111 kuna nyumba au sehemu ya nyumba 5007 ambazo zinamilikiwa na waliokuwa wamiliki wa awali au na wale ambao walikuwa wanunuzi.

“Sasa nyumba hizi kuna baadhi ambazo zinapaswa kurejeshwa katika Shirika la Nyumba la Taifa pale mmiliki aliyepewa hiyo sehemu anapofariki na nyumba zingine hazipaswi kurejeshwa katika Shirika la Nyumba la Taifa.

“Wanaendelea kuzitumia, sasa nitoe wito kwa wale wote ambao wamepewa haki ya kutumia nyumba hizo kwa maisha yao tu, ni vizuri ndugu zao, jamaa kwa maana ya wanaohusika na hao waliopewa haki hiyo pale inapotokea mtu huyu amefariki ni wajibu wao kurejesha nyumba hizo katika Shirika la Nyumba la Taifa.

“Sisi katika shirika tunaendelea kuzikagua nyumba zetu na si vizuri kuanza kupita na kuanza kuulizia fulani yupo hai ama hayupo hai.

"Kinachotakiwa ni kwamba wale watu wa mtu aliyepewa haki hiyo ni vizuri wakaweza kutii sheria na kuhakikisha kwamba wanarejesha nyumba hizo kwa mujibu wa sheria ili ziweze kupangishwa kwa wao wenyewe wakiomba au ziweze kupangishwa kwa Watanzania wengine.

“Huo ndiyo wito wa shirika, na tunaendelea kukagua nyumba hizo ili kuhakiki wanaokaa nyumba hizo kama ndiyo hasa wanaendelea kukaa katika nyumba hizo kwa muda wa maisha yao tu,”amefafanua kwa kina Meneja wa Habari na Mawasiliano NHC, Muungano Saguya.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news