Panga vema mikakati

NA LWAGA MWAMBANDE

NI wazi kuwa, kila mmoja wetu anao wajibu wa kujenga tabia ya kujiwekea malengo makubwa kwa manufaa ya sasa na baadaye.

Picha na apeejay

Mara nyingi, yafaa ukumbuke kuwa, unachokitaka kukifanya sasa tayari kuna watu wameshafanikiwa,hivyo kwako pia kukifanikisha inawezekana tena huenda kwa mafanikio zaidi.

Aidha, uwezo wetu wa kufanya jambo flani unakomea pale fikra na malengo yetu yanapoishia. Ndiyo maana, ukipanga vema mikakati yako ni rahisi zaidi kuziendea ndoto zako kwa haraka na pengine kwa kipindi kifupi.

Yafaa kutambua kuwa, mafanikio katika maisha sio kitu cha siku moja bali ni namna ya kuishi na matokeo ya juhudi na jitihada ya kutimiza kazi na mipango midogo midogo ambayo inaendana na lengo kubwa.

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasisitiza kuwa, mwaka 2024 tumeuanza, hivyo tambua kuwa,mipango na mikakati mizuri ndio inayofanya malengo ya mtu kutimia. Endelea;

1.Mikakati yako wewe, Mungu akikuongoza,
Usijidharau wewe, ndoto utazitimiza,
Ndoto ndogo usigawe, anzia kuzitimiza,
Panga vema mikakati, malengo uyatimize.

2.Mwaka wetu huu mpya, wenyewe mejituliza,
Ni wewe kupiga chafya, kwa yale unayowaza,
Kwa maisha kwako afya, fanya ya kujiongeza,
Panga vema mikakati, malengo uyatimize.

3.Mwaka huu uwe chachu, ndoto yako kutimiza,
Akili iwe na uchu, jambo la kutekeleza,
Shughulika kama Zuchu, huko mbele tatokeza,
Panga vema mikakati, malengo uyatimize.

4.Sijiulize ulize, muda ndio wamaliza,
Ikibidi jiapize, yako uanze sogeza,
Wewe usijilemaze, jiamini unaweza,
Panga vema mikakati, malengo uyatimize.

5.Heri mwaka mpya huu, vile Mungu katutunza,
Pendo lake kwetu kuu, hajataka tupunguza,
Apenda yetu makuu, tuweze yatekeleza,
Panga vema mikakati, malengo uyatimize.

Lwaga Mwambande
lwagha@gmail.com

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news