Rais Dkt.Mwinyi afungua Kituo cha Huduma za Dharura na Maabara,atoa wito kwa wananchi

ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Mwinyi amewataka wananchi kuvitumia vituo vya afya ili kupunguza msongamano wa wagonjwa katika Hospitali za Rufaa.
Wito huo ameutoa katika uwanja wa Mwakakogwa Makunduchi Wilaya ya Kusini Unguja wakati akifungua Kituo cha Huduma za Dharura na Maabara.

Aidha, ameitaka Wizara ya Afya kuhakikisha inaweka wafanyakazi wenye ujuzi ili kutoa huduma bora kwa wagonjwa.

Amebainisha kuwa, ujenzi huo ni miongoni mwa juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha miundombinu bora ya upatikanaji wa huduma za Afya nchini.
Rais Dkt.Mwinyi ameeleza kuwa, Serikali itaendelea kujenga hospitali za mikoa na kuweka vifaa tiba vya kisasa ili kusogeza huduma za afya karibu na jamii.

Ameongeza kuwa, ujenzi wa miundombinu kama hiyo na uwepo wa huduma za Afya kwa ngazi ya jamii umesaidia kupunguza vifo vya mama na mtoto pamoja na maradhi yasiyoambukiza.
Naye, Naibu Waziri wa Afya, Mhe. Hassan Khamis Hafidh amesema kuwa huduma za afya zimeongezeka kwenye kituo hicho ikiwemo vitengo vya huduma za uchunguzi wa dharura.

Aidha, amewataka watendaji wa Wizara ya Afya kutoa huduma bora na za uhakika ili wananchi waweze kunufaika.

Akitoa taarifa ya kitaalamu Kaimu Katibu Mkuu ambae pia ni Mkurugenzi Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Amour Suleiman amesema kuwa awali kulikuwa hakuna jengo la huduma za uchunguzi wa dharura linalokwenda na wakati jambo ambalo lilileta usumbufu kwa wagonjwa.
Amesema kuwa,kutokana na changamoto hiyo ilipelekea kujengwa kituo hicho kupitia ufadhili wa Lady Fatma Foundation Trust kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news