ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Mwinyi ametembelea banda la Benki Kuu ya Tanzania katika Maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya Zanzibar yanayofanyika katika viwanja vya Fumba, Kisiwani Unguja kuanzia Januari 7-19, 2024.
Kupitia Maonesho hayo Benki Kuu inaelimisha wananchi kuhusu sera za uchumi na fedha, uwekezaji katika dhamana za serikali, usimamizi wa fedha binafsi, akiba na mkopo.
Sambamba na namna BoT inawalinda watumiaji wa huduma za fedha,utunzaji sahihi wa noti na utambuzi wa alama za usalama, mifumo ya malipo ya taifa na namna Bodi ya Bima ya Amana inavyokinga amana za wateja wa benki na taasisi za fedha.
Wakati huo huo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi amesema, Serikali ina mpango mzuri wa kujenga majengo ya kisasa ya Maonesho ya Biashara na kuwa kivutio kikubwa kwa wadau wa biashara, taasisi na mashirika ya kitaifa na kimataifa.
Mheshimiwa Rais amesema hayo Januari 10,2024 alipofungua Maonesho ya 10 ya Biashara Zanzibar na kuufungua rasmi uwanja huo mpya wa Maonesho Dimani Mkoa wa Mjini Magharibi katika shamrashamraza miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Aidha, Rais Dkt.Mwinyi ameeleza kuwa Maonesho hayo yameshirikisha washiriki wengi kutoka taasisi za Serikali, sekta binafsi, wafanyabiashara wakubwa na wadogo pamoja na wajasiriamali.
Vilevile Rais Dkt.Mwinyi ameitaka Wizara ya Biashara na Maendeleo ya viwanda kulitangaza eneo jipya hilo la maonesho na kulifanya kuwa kimataifa.
Halikadhalika Rais Dkt.Mwinyi amekubali ombi la kuanzishwa kitengo maalum kuendesha na kusimamia viwanja hivyo vipya.
Kwa upande mwingine Rais Dkt.Mwinyi ameipongeza Wizara ya Biashara na Maendeleo ya viwanda kwa kuendelea kufanya miradi mikubwa ya maendeleo na kuacha alama , pia amewataka kushughulikia maendeleo ya viwanda nchini.