ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi amesema, kazi inayofanywa na taasisi za elimu ya juu ni kielelezo cha mchango wa sekta binafsi kuchangia maendeleo ya Zanzibar kwa kuandaa wataalamu wa fani mbalimbali.
Rais Dkt.Mwinyi amesema hayo Januari 27,2024 katika Mahafali ya 23 ya Chuo Kikuu cha Abdulrahman Al -Sumait Chukwani Mkoa wa Mjini Magharibi.
Aidha,Rais Dkt.Mwinyi amepongeza juhudi zinazofanywa na Chuo hicho kinachomilikiwa na Shirika la Direct Aid ya Kuwait kwa mchango wake katika maendeleo ya sekta ya elimu Zanzibar tangu kuanzishwa kwake 1998.
Rais Dkt.Mwinyi amevihimiza vyuo kujikita katika utafiti utakaotoa ufumbuzi wa changamoto zinazoikabili jamii kwa kushirikiana na taasisi na idara mbalimbali za Serikali.
Kwa upande mwingine Rais Dk.Mwinyi amevitaka vyuo kikuu kuongeza programu zinazoakisi mahitaji ya nchi ikiwemo zinazohusu uchumi wa buluu.
Mahafali hayo yamehudhuriwa na Mkuu wa Chuo cha Abdulrahman Al-Sait, Rais mstaafu Mhe.Dkt.Amani Abeid Karume, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Mhe. Lela Mohamed Mussa, Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Mhe.Idrissa Kitwana Mustafa pamoja na viongozi mbalimbali wa Serikali, wa Dini na Vyombo vya ulinzi na usalama.
Tags
Abdulrahman Al -Sumait Chukwani
Dkt.Hussein Ali Mwinyi
Dr.Amani Abeid Karume
Habari
Serikali ya Awamu ya Nane Zanzibar
Zanzibar News