DAR ES SALAAM-Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajia kufanya ziara ya kitaifa Vatican kuanzia Februari 11 hadi 12, 2024.
Ni kufuatia mwaliko wa Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki Duniani, Baba Mtakatifu Francis.
Hayo yameelezwa Januari 21,2024 na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,Mheshimiwa January Makamba wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Amesema, dhumuni la ziara hiyo ni kuimarisha ushirikiano wa uwili kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Vatican.
“Itakumbukwa mwaka 2016 Hayati Dkt. John Pombe Magufuli, alimwalika Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki Duniani, yaani Baba Mtakatifu Francis kutembelea Tanzania.
"Hata hivyo, kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo za kiafya ziara hiyo haikuwezekana na badala yake kwa wakati huu, Rais Samia amealikwa na Kiongozi huyo kufanya ziara Vatican.
“Akiwa Vatican, Rais atakutana kwa mazungumzo na Baba Mtakatifu Francis pamoja na Katibu wa Vatican, Pietro Parolin.
"Lakini kabla ya ziara ya Vatican Rais pia atafanya ziara ya Kitaifa nchini Indonesia kuanzia Januari 24 hadi 26 kufuatia mwaliko wa Joko Widodo, Rais wa Jamhuri ya Indonesia, ziara hii ya Kitaifa inafuatia ziara ya Kitaifa ya Rais Joko Widodo aliyoifanya Tanzania mwezi Agosti 2023,"amebainisha Mheshimiwa Makamba.
Pia, amesema Rais Dkt.Samia atafanya ziara ya Kitaifa nchini Norway kuanzia Februari 13 hadi 14, 2024, kufuatia mwaliko kutoka kwa Mfalme Herald wa Norway na Malkia Sonja.
Ziara hiyo inakuja, ikiwa ni miaka 60 tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Taifa hilo.