Rhobi Samwelly abisha hodi kwa wajane mkoani Mara, asisitiza lazima wainuke kiuchumi

NA FRESHA KINASA

WANAWAKE wajane wanaojishughulisha na ujasiriamali katika Manispaa ya Musoma mkoani Mara wametakiwa kuwa wabunifu na kutumia vyema fursa mbalimbali za kiuchumi zinazopatikana na kuwazunguka kusudi wakuze biashara zao na wainuke kiuchumi.
Hayo yamesemwa leo Januari 16, 2024 na Mkurugenzi wa Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania, Rhobi Samwelly wakati akitoa mafunzo ya ujasiriamali kwa wanawake hao yaliyofanyika ukumbi wa Musoma Club. Ambapo zaidi ya wajasiriamali 200 wamehudhuria mafunzo hayo.

Mafunzo hayo yameendeshwa na shirika hilo kupitia Programu ya Erasto Widows Empowerment Programme kwa kushirikiana na Benki ya CRDB kupitia Programu ya EMBEJU ambapo wanatarajia kunufaika na mikopo waendeleze biashara zao.

Rhobi amesema kuwa, iwapo wakitumia vyema fursa ya mikopo kwa ufanisi ambayo wanatarajia kupewa na CRDB watakuza biashara zao, na hivyo kuwa na kipato cha uhakika kitakachowasaidia kuhudumia familia zao na kufanya maendeleo huku akiwaomba wasijione wanyonge.
Ameongeza kuwa, kupitia programu ya Erasto Widows Empowerment Programme iliyo chini ya Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania anatarajia kuwafikia wanawake wengi wa Mkoa wa Mara kwa kuwapa elimu ya ujasiriamali pamoja na kuwaunganisha na fursa za mikopo ili kuona kundi la wanawake linaimarika kiuchumi.

"Tumieni fursa ya mikopo nafuu ambayo haina masharti magumu mtakayopewa na CRDB kusudi mkuze biashara zenu, lakini pia niwaombe muwe wabunifu mnapofanya biashara zenu pamoja na nidhamu ya fedha haitafaa mnapewa mikopo mnakwenda kuitumia kinyume na malengo, "amesema Rhobi.

Victoria Wandiba ni mama mjane na mjasiriamali anayeishi Mtaa wa Nyabisare Manispaa ya Musoma akizungumza kwa niaba ya wajasiriamali hao, amesema kuwa, baadhi ya wajane wamekuwa wakiishi maisha ya tabu na kushindwa kujishughulisha kiuchumi kutokana na kukosa mitaji.
"Mafunzo haya ya ujasiliamali yamekuja muda mwafaka kwetu wajasiriamali tumepata elimu na mbinu za kuendesha biashara zetu. Lakini pia tumshukuru Rhobi kutuunganisha na CRDB ambao watatupa mikopo kuendeleza biashara zetu kupitia vikundi.

"Kwa hiyo, Wajane ambao bado hawajaanza kujishughulisha na Wananguvu wabuni biashara ndogondogo wawe na sehemu ya kujipatia kipato,"amesema Victoria.

Kupitia Programu ya EMBEJU mikopo kwa wajasiriamali hao itatolewa bila riba ambapo kutakuwa na ada ya asilimia sita ya mkopo, na asilimia moja kwa ajili ya malipo ya bima. Na kikundi kitakuwa dhamana kwa Mkopaji.

Mikopo hiyo itatolewa kupitia vikundi kwa kumkopesha mjasiriamali mmoja mmoja akiwa ndani ya kikundi ili kuhakikisha kwamba wanainuka kiuchumi kwa kuendeleza biashara zao ambazo tayari wanazo. Huku wanufaika ni Wanawake wajasiriamali kuanzia miaka 18 hadi miaka 60 na mwisho wa kurejesha mkopo ni mwaka mmoja.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news