Saa chache baada ya TCAA kutangaza kuipiga marufuku Kenya Airways,Waziri Makamba na Mudavadi waingilia kati

NA DIRAMAKINI 

SAA chache baada ya Mamlaka ya Usimamizi wa Anga Tanzania (TCAA) kutangaza kulifutia Shirika la KenyaAirways kibali cha kufanya shughuli zake nchini kuanzia Januari 22, mwaka huu, mawaziri wa Mambo ya Nje wa pande hizo mbili wameingilia kati kutafuta suluhu ya haraka.
Taarifa iliyotolewa na Mkurungezi Mkuu wa TCAA, Hamza Johari imesema kuwa, mamlaka hiyo imefikia uamuzi huo kama mrejesho wa nchi ya Kenya kuinyima kibali Tanzania kusafirisha mizigo kwa njia anga kutokea nchini humo kwenda maeneo mbalimbali duniani.
Aidha,Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mheshimiwa January Makamba amesema, amefanya mazungumzo na Waziri mwenzake anayeshughulikia masuala ya kigeni nchini Kenya, Musalia Mudavadi na wamekubaliana kumaliza sakata linaloendelea ikiwemo zuio la ndege za Kenya Airways kutua Tanzania.

Waziri Makamba amesema, kwa mamlaka waliyonayo wamekubaliana kumaliza jambo hilo ndani ya siku tatu.

"Nimezungumza na mwenzangu Musalia Mudavadi.Tunakubali kwamba vikwazo vya usafiri wa anga kati ya nchi zetu na kutoka nchi yoyote hadi nchi nyingine havipaswi kuwepo.

"Pamoja na mamlaka husika, tumeazimia kusuluhisha jambo hili, kulingana na makubaliano yaliyopo, ndani ya siku tatu."

Kupitia ukurasa wake wa Twitter, Mheshimiwa Mudavadi amefafanua kuwa,"jioni hii nimezungumza na Mheshimiwa January Makamba (Mb), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuhusu uamuzi wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania kutengua idhini ya Shirika la Ndege la Kenya Airways kuendesha safari za abiria kati ya Nairobi na Dar es Salaam, kuanzia tarehe 22 Januari 2024. 

"Tumekubaliana kwa pamoja kwamba mamlaka zetu za usafiri wa anga zitafanya kazi pamoja ili suala hilo litatuliwe kwa amani ndani ya siku tatu zijazo. Kwa hivyo kusiwe na sababu ya kutisha."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news