NA LWAGA MWAMBANDE
REJEA Bibilia Takatifu katika kitabu cha Ufunuo wa Yohana 9:6 neno la Mungu linasema, "Na siku zile wanadamu watatafuta mauti, wala hawataiona kamwe. Nao watatamani kufa, nayo mauti itawakimbia."
Pia, rejea Ufunuo wa Yohana 20:14 neno la Mungu linasema, "Mauti na kuzimu zikatupwa katika lile ziwa la moto. Hii ndiyo mauti ya pili, yaani, hilo ziwa la moto."
Ni wazi kwa tafakari hiyo ndogo utabaini kuwa, mauti ni roho na roho yoyote ina kinywa, miguu, mikono, akili na kiwiliwili (lakini cha rohoni ambacho hakiwezi kuonekana kwa macho ya nyama) ndio maana inaweza kutembea na kukimbia.
Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anafafanua kuwa, yakupasa usitafakari njia zako na kumrejea Mungu, la si hivyo mauti malipo yako ni suala la muda tu. Endelea;
1.Waoga wasoamini, na wale wachukizao,
Neno lasema amini, wanayo malipo yao,
Mungu wampiga chini, wanafwata njia zao,
Mauti yao ya pili, ziwa liwakalo moto.
2.Wauaji na wazinzi, ambao dhambi ni zao,
Uchawi wanaoenzi, sanamu ibada zao,
Kwa uongo ni watunzi, katika maisha yao,
Mauti yao ya pili, ziwa liwakalo moto.
3.Kumbe Mungu kumwamini, mbele yako ni mafao,
Na hata kutomwamini, utayapata mazao,
Sasa akili kichwani, kwetu sote hata kwao,
Mauti yao ya pili, ziwa liwakalo moto.
4.Ukiishi duniani, hebu jiepushe nao,
Neno liwe ni amini, ubaya achana nao,
Tenga nafasi mbinguni, wenye dhambi siyo kwao,
Mauti yao ya pili, ziwa liwakalo moto.
5.Ufanye hesabu zako, wafanye hesabu zao,
Mrudie Mungu wako, wala siwafwate wao,
Wengine huko waliko, toka zamani ni kwao,
Mauti yao ya pili, ziwa liwakalo moto.
6.Mungu kimkaribia, atakuambia wao,
Naye takukaribia, awe nawe kama ngome,
Aongoze yako njia, hadi ya kwake makao,
Mauti yao ya pili, ziwa liwakalo moto.
7.Lazaro naye tajiri, nasi tujifunze kwao,
Tajiri chake kiburi, Lazaro miisho yao,
Uduniani ngangari, huko lilia kivyao,
Mauti yao ya pili, ziwa liwakalo moto.
8.Lazaro umasikini, kwa Mungu ana makao,
Liteseka duniani, walivyomcheka hao,
Ila kwa Mungu mbinguni, raha yake siyo yao,
Mauti yao ya pili, ziwa liwakalo moto.
9.Na pale msalabani, Yesu wahalifu hao
Mmoja yule muhuni, dhihaka, kama yao,
Mwingine jishusha chini, kitubu makosa yao,
Mauti yao ya pili, ziwa liwakalo moto.
10.Jibu Yesu bado lipo, kampatia makao,
Hilo hata kwako lipo, acha mbaya njia zao,
Ujue pale alipo, nawe unayo makao,
Mauti yao ya pili, ziwa liwakalo moto.
11.Mwokozi aja upesi, ujio kwetu na kwao,
Mwisho wa kwao ni hasi, wale dhambi wafanyao,
Mwisho chanya kwetu sisi, tusoishi kama wao,
Mauti yao ya pili, ziwa liwakalo moto.
(Ufunuo wa Yohana 21:8)
Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602