Sekta ya Mawasiliano ni kichocheo cha maendeleo nchini-Waziri Mkuu



*Asema ina mchango mkubwa katika kuimarisha uchumi, ulinzi na usalama

LINDI-Ibara 18 (2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inasema kuwa “Kila raia anayo haki ya kupewa taarifa wakati wote kuhusu matukio mbalimbali nchini na duniani kote ambayo ni muhimu kwa maisha na shughuli za wananchi, na pia juu ya masuala muhimu kwa jamii”. 

Hivyo suala la wananchi kupata habari ni muhimu kwani ni chachu ya maendeleo na pia ni takwa la kikatiba.
Ni ukweli usiopingika kuwa huduma bora za mawasiliano ni muhimu sana kwani ni kichocheo katika kuleta maendeleo ya jamii na nchi nzima kwa ujumla na umuhimu huo unadhirika kutokana na mchango wake katika nyanja za kiuchumi, kisiasa, kijamii na pia katika masuala ya ulinzi na usalama.

Vilevile, huduma ya mawasiliano ni chachu ya ukuaji wa sekta nyingine za kiuchumi kutokana na ukweli kwamba mafanikio katika sekta mbalimbali huchangiwa kwa kiasi kikubwa na uwepo wa huduma za uhakika za mawasiliano.

Hatua hiyo inatokana na maboresho makubwa yaliyofanywa na Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika sekta hiyo, akiamini kwamba kupitia mawasiliano taarifa mbalimbali muhimu za Serikali na sekta binafsi zinawafikia walengwa wote wakiwemo wananchi kwa wakati na kwa ufanisi na hatimaye kuleta tija inayokusudiwa.

Januari 6, mwaka huu, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alizindua studio za Redio Jamii- Ruangwa ambayo itaharakisha maendeleo ya wana Ruangwa. 

“Tukio la leo ni hatua muhimu katika kuwapatia wananchi haki yao ya kikatiba ya kupata habari. Ni matumaini yangu kwamba Wana-Ruangwa pamoja na wananchi wa maeneo jirani watanufaika na huduma za utangazaji zitakazopatikana kupitia redio hii.”

Mheshimiwa Majaliwa alisema Sekta ya utangazaji ni muhimu sana katika dunia ya sasa ya kidigitali ambapo upashanaji wa habari umekuwa ni msingi wa ukuaji wa uchumi na kuwa chachu ya maendeleo ya mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

“Huu ndio msukumo wa Serikali yetu katika kuhakikisha uwepo wa miundombinu bora ya mawasiliano yatakayowezesha jamii yote ya Watanzania kupata habari muhimu za kijamii, kitaifa na kimataifa ambazo zitawapa maarifa na utayari wa kufanya shughuli mbalimbali za maendeleo ya Taifa letu.”

Alisema redio hiyo inakusudiwa kusikika katika maeneo ya Wilaya ya Ruangwa, kutokana na uwezo wa mitambo masafa yatafika hadi maeneo ya wilaya za Masasi, Liwale na Kilwa, hivyo kuwawezesha wananchi wengi zaidi kufikiwa na huduma hiyo muhimu kwani kupitia matangazo ya redio hiyo wataweza kufahamu mambo yanayoendelea katika sehemu mbalimbali nchini na duniani kwa ujumla.

Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa alisema ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya Mwaka 2020/2025; Ibara ya 125 (a) imeielekeza Serikali kuendelea kutekeleza Sheria ya Huduma za Habari na. 12 ya Mwaka 2016 ili kuhakikisha kuwa wananchi wanapata taarifa sahihi kwa urahisi zaidi na kwa wakati.

Waziri Mkuu aliongeza kuwa uzinduzi wa kituo hiko ni sehemu ya utekelezaji wa matakwa ya Ilani ambayo imedhamiria kuhakikisha kuwa sekta ya habari inaboreshwa ili kuwaongezea wananchi fursa ya kupata habari kwa kuongeza wigo wa upashanaji wa habari.

Alisema, huduma ya mawasiliano ni chachu ya ukuaji wa sekta nyingine za kiuchumi, kwa kupitia mawasiliano taarifa mbalimbali muhimu za Serikali na sekta binafsi zinawafikia walengwa wote wakiwemo wananchi kwa wakati na kwa ufanisi na hatimaye kuleta tija inayokusudiwa.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu aliwataka watumishi wa Redio Jamii- Ruangwa wahakikishe wanatunza na kutumia kwa uangalifu vifaa vilivyonunuliwa ili viweze kudumu kwa muda mrefu na pia wasikilizaji waendelee kunufaika na huduma za utangazaji za Redio hiyo. "Vyombo vyote vya Habari zikiwemo redio na luninga fanyeni utafiti kabla ya kufikisha habari kwa wasikilizaji na watazamaji."

Pia, Waziri Mkuu aliwasisitiza Watendaji wa Halmashauri zote watumie fursa ya uwepo wa redio kufikisha matangazo muhimu kwa wananchi wa maeneo yanayofikiwa na usikivu. “Mwaka huu tunatarajia kuwa na uchaguzi wa Serikali za Mitaa, tumieni redio za jamii kuwapa wananchi taarifa muhimu zinazohusiana na mchakato huo muhimu kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.”

Kwa upande wake, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye ametoa wito kwa watumishi wa redio hiyo wahakikishe wanakwenda hadi vijijini kwa ajili ya kuandaa vipindi mbalimbali vya maendeleo ya wananchi.

Pia, Waziri Nape alisema Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknoljia ya Habari kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) imekuwa ikitekeleza miradi mbalimbali ya mawasiliano nchini ambayo lengo lake ni kuhakikisha wananchi wote hususan waishio maeneo ya pembezoni ikiwemo mipakani wanapata huduma ya mawasiliano.

Alisema miradi mingine inayoendelea kutekelezwa kuwa ni pamoja na ya kuboresha usikivu wa redio maeneo ya mipakani ambao umekuwa ukitekelezwa na TBC na UCSAF katika maeneo mbalimbali ya nchini ili kuhakikisha Watanzania wote wanapata haki yao ya kikatiba ya kupata habari bila kujali maeneo wanayoishi.

Naye, Afisa Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), Justina Mashiba amesema vifaa vilivyofungwa katika studio hizo ni vya kisasa na vina uwezo wa kufika kilomita 200 kwa pande zote. "Redio hiyo inasikika katika wilaya za Liwale, Nachingwea, Kilwa na Masasi."

Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa, Bw. Frank Chonya alisema dhamira ya redio hiyo ni kuwaelimisha, kuwaburudisha Wana-Ruangwa, hivyo aliishukuru Serikali kwa kutoa zaidi ya shilingi milioni 550 kwa ajili ya uboreshaji wa redio hiyo.

Kwa upande wao wakazi wa wilaya ya Ruangwa wakizungumza baada ya uzinduzi huo waliishukuru Serikali kwa kuwafikishia huduma za amawasiliano katika wilaya yao. Walisema awali hakukuwa na usikivu mzuri wa redio na hivyo kusababisha kukosa baadhi ya taarifa.

Wakazi hao walisema mbali na maboresho makubwa yaliyofanywa katika redio pia kwa sasa mawasiliano kwa kupitia simu za mkononi nayo yameboreshwa na sasa wanawasiliana vizuri na jamaa zao. “Mfano sisi wakazi wa tarafa ya Mandawa miaka ya nyumba hatukuwa na mawasiliano ya simu lakini kwa sasa tunayo na tunazungumza vizuri.”

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news