ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi amesema, Serikali imejenga skuli za kisasa za ghorofa mijini, vijijini pamoja na maeneo ya visiwa vidogovidogo ikiwemo Gamba, Kojani, Tumbatu.
Amesema ahadi ya CCM iliandika kujenga mabanda ya skuli, ambapo Serikali ya Awamu ya Nane inaendelea na kujenga skuli za kisasa za ghorofa pamoja na ujenzi wa maeneo 25 kwa mwaka wa fedha 2023/24.
Rais Dkt.Mwinyi amesema hayo Januari 3, 2023 alipoweka Jiwe la Msingi la ujenzi wa Skuli ya Sekondari Maziwang'ombe Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba katika shamrashamra za Maadhimisho ya Miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Aidha, Rais Dkt.Mwinyi ameeleza kuwa, Serikali inakusudia kuajiri walimu wapya 1,500 mwaka huu na kufanyia kazi masuala ya posho na mishahara yao.
Halikadhalika Rais Dkt.Mwinyi amesema, Serikali inafanya mageuzi katika mitaala ikiwemo elimu ya ujuzi pamoja na kuanzisha Tume ya Watumishi kwa walimu ili kutatua changamoto zao.
Kwa upande mwingine Rais Dkt.Mwinyi amesema, lengo la Serikali ni kuhakikisha wanafunzi wanaingia asubuhi tu nchi nzima badala ya utaratibu wa kuingia kwa zamu pia kwa kila darasa wanafunzi wasizidi 45.