ZANZIBAR-Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi imeanza ugawaji wa vifaranga vya samaki aina ya mwatiko kwa wafugaji wa samaki Unguja na Pemba ili kuongeza uzalishaji.
Akizungumza mara baada ya kumaliza zoezi la ugawaji wa vifaranga hivyo huko Beit -el Rais Wilaya ya Magharib 'A', Katibu Mkuu Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi, Dkt. Aboud Suleiman Jumbe amesema, lengo la kugawa vifaranga hivyo kwa wafugaji ni kuona Zanzibar inakuwa na samaki wa kutosha ambao watatosheleza mahitaji kwa wananchi.
Dkt. Aboud amesema,ili kazi ya ufugaji wa samaki iweze kuendelea vyema wafugaji wamepatiwa mafunzo ya kitaalamu ya kutumia mabwawa pamoja na kutumia teknolojia mpya ya ufugaji.
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi na Maliasili za Bahari, Dkt. Zakaria Ali Khamis amesema, utafiti wa samaki aina ya mwatiko,matango bahari na kaa tope umefanyika katika maeneo mbalimbali.
Amesema,wizara itaendelea na tafiti za maliasili za baharini ili kwenda sambamba na kipaumbele cha Serikali cha kuongeza uzalishaji wa samaki hapa Zanzibar.
Naye Mkurugenzi wa Maendeleo ya Uvuvi na Mazao ya Baharini, Dkt. Salum Soud Hamed amesema, watahakikisha Zanzibar inakuwa mfano bora kwa Afrika na duniani kote katika uzalishaji wa samaki ili kutosheleza mahitaji hapa nchini.
Mratibu wa Mradi wa Kuendeleza Kilimo na Uvuvi (IFAD), Amina Hussein Khamis amesema, mradi huo unaendelea kuimarisha miundombinu na kutoa taaluma ya ufugaji wa samaki pamoja na kuwataka wafugaji kujitokeza kwa wingi kuchukua vifaranga ili kuendelea na ufugaji na kujiongezea kipato.
Kwa upande wake Mtaalamu wa shughuli za Ufugaji wa Mazao ya Baharini,Fatma Suleiman Ali kutoka Idara ya Utafiti wa Uvuvi na Maliasili za Bahari (ZAFIRI) amewataka wafugaji hao kutumia njia waliyowekewa kitaalamu ya kuwahifadhi vifaranga katika vizimba walivojengewa katika mabwawa ya kufugia mara baada ya kukabidhiwa kwa ajili ya usalama wa maisha ya vifaranga hivyo.