Serikali yatoa maelekezo kwa wananchi kuhusu madhara yatokanayo na mvua

MWANZA-Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi amewataka wananchi kuzingatia na kufuata taratibu zinazotolewa na Serikali ili kuweza kukabiliana na madhara yatokananyo na mvua hasa za El nino kuweza kuokoa maisha na mali zao.
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi (katikati) na wataalam kutoka Ofisi ya Mkoa wa Mwanza, TARURA, TANROADS na Ofisi yake wakati wa ziara ya kutembelea baadhi ya maeneo yaliyoathiriwa na Mvua zinazoendela kunyesha mkoani Mwanza.

Ameyasema hayo Januari 20, 2024, Jijini Mwanza alipokuwa katika ziara ya kukagua hali ya Mafuriko katika Jiji hilo ambapo mvua la El nino zinazoendelea zimeleta athari mbalimbali na kuharibu miundombinu pamoja na mali za watu.

Dkt. Yonazi amesema ni muhimu sana wananchi kuwa wazalendo na kufuata maelekezo ya serikali kwa sababu suala zima la uokoaji ni gharama.

“Suala hili ni gharama kwa Serikali,lakini pia inaweza kugharimu maisha hivyo ni muhimu sana pale ambapo tumeelekezwa na Serikali kufuata taratibu tuweze kufuata taratibu,” alisisitiza.
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) katika eneo maarufu kwa jina la Daraja la Masai, lililopo katika Mtaa wa uhuru Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza mara baada ya kumaliza ziara yake ya kukagua maeneo yaliyoathiriwa na mvua zinazoendelea kunyesha.

Katibu Mkuu Dkt. Yonazi amebainisha kuwa kwa wananchi ambao wameelekezwa kuhama katika maeneo hatarishi waweze kuhama ili waweze kulinda maisha yao, mali zao na maisha ya jamii kwa ujumla na ametoa wito kwa wananchi kote nchini kufuata taratibu, miongozo na maelekezo halali ya Serikali na ndiyo namna ya kujilinda dhidi ya mafuriko na majanga.

Amewataka pia wananchi kushiriki katika miradi mikubwa akitolea mfano mradi wa ujenzi wa kingo za mto Nyamilongo unaopita katika wilaya ya Nyamagana ili maji yake yasiende katika makazi ya watu na kuharibu mali nyingine na kufahamu kwamba ushiriki wao utaleta faida katika maana ya kutunza mali zao, mali za asili na kuhakikisha kwamba maisha yanaendelea vizuri.
Baadhi ya wataalam kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu wakiwa katika kikao kabla kuanza kwa ziara ya Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi ya kutembelea baadhi ya maeneo yaliyoathiriwa na Mvua zinazoendela kunyesha mkoani Mwanza.

Katika hatua nyingine,Dkt. Yonazi amewaasa watumishi wa umma kufuata utaratibu hasa katika kusimamia suala zima la ujenzi holela, kwani unapofanyika ujenzi holela ni rahisi sana kupata madhara.

“Ili kuweza kuwa na makazi bora kwa wananchi wetu ni vizuri kuhakikisha maisha hayahatarishwi na mafuriko na hata yanapotokea mafuriko inakuwa rahisi kuokoa,” amesema Dkt.Yonazi.
Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza, Bw. Baladya Eliakama, akizungumza kuhusiana na madhara ya mvua zinaoendelea kunyesha katika mkoa wa Mwanza kabla ya kuanza kwa ziara ya Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi ya kutembelea maeneo yaliyoathiriwa na mvua hizo.

Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, Bw. Balandya Elikana amesema, mvua hizi za El nino kwa baadhi ya maeneo katika mkoa wa Mwanza zimeleta uharibifu wa baadhi ya miundombinu kama vile madaraja na Barabara.

Aidha,amepongeza Wakala wa Barabara mijini na vijijini (TARURA) mkoani Mwanza kwa kuendelea kufanya kazi kubwa ya kuhakikisha kwamba miundombinu hiyo inarejea katika hali yake ya kawaida.
Muonekano wa sehemu za kingo za miundombinu ya Daraja unapopita mto Nyamilongo Wilayani Nyamagana lilivyoharibiwa na mvua zinazoendela kunyesha mkoani Mwanza.

Sambamba na hilo amesema suala la mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu mkoani humo, ambapo amesema ulianzia katika Wilaya ya Magu na kufika katika wilaya ya Ilemela na Nyamagana ambapo Serikali ya mkoa kwa kiasi kikubwa imechukua hatua, tahadhari pamoja na kudhibiti.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news