DAR ES SALAAM-Mamlaka ya Usafiri wa Anga nchini Kenya (KCAA) imeondoa zuio la ndege ya mizigo ya Air Tanzania kusafirisha mizigo kutoka jijini Nairobi kwenda mataifa mengine.
Uamuzi huo umefikiwa ikiwa ni saa kadhaa baada ya Mamlaka ya Usafri wa Anga nchini Tanzania (TCAA) kutangaza nia ya kuzuia safari za ndege za abiria za Shirika la Ndege la Kenya (Kenya Airways).
Uamuzi huo ulipangwa kuanza Januari 22, 2024 uliwekwa kando baada ya mawaziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kenya na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kukubaliana kutafuta suluhu ya mgogoro huo katika kipindi cha siku tatu. Taarifa ya Mamlaka ya Usafiri wa Anga nchini Tanzania iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu, Hamza Johari imesema Kenya imeruhusu ndege ya Mizigo ya ATCL kuanza kusafirisha mizigo kutokea Nairobi kuanzia leo, Januari 16.
Aidha,baada ya uamuzi huo, Johari amesema mamlaka nchini Tanzania zinaondoa zuio la ndege za abiria za KQ kuingia katika anga la Tanzania.