Tanzania kushiriki mkutano wa Mining Indaba 2024 nchini Afrika Kusini

DODOMA-Wizara ya Madini imewaeleza Watanzania na wadau wa Sekta ya Madini kuwa, kwa mara ya kwanza kwa kushirikiana na Chemba ya Migodi inayowakilisha Sekta Binafsi zitashiriki kwa pamoja kuiwakilisha Tanzania katika Mkutano wa Madini barani Afrika wa Mining Indaba unaofanyika mwezi Februari kila mwaka nchini Afrika Kusini.
Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Januari 22,2024 na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,Wizara ya Madini.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mkutano huo utafanyika tarehe 5 hadi 8 Februari, 2024 katika jiji la Cape Town ukiwa ni sehemu muhimu ya kujenga uhusiano na kuongeza wigo wa kibiashara katika sekta ya madini.

Pia, umeendelea kutumika kama eneo la kutafuta wawekezaji, mitaji, teknolojia, wabia, biashara, kubadilishana uzoefu na kujifunza kuhusu usimamizi endelevu na ukuzaji wa Sekta ya Madini barani Afrika.

Tanzania itashiriki chini ya kaulimbiu Ustawi Imara kwa Kuendeleza Uwekezaji katika Sekta ya Madini, Kaulimbiu hii inachochea jitihada za Serikali ya Tanzania kutekeleza vipaumbele vya Wizara katika kuendeleza madini muhimu na mkakati ikiwemo Dira ya 2030:

"Madini ni Maisha na Utajiri'', inayolenga kupata taarifa za kina za kijiofizikia kufikia asilimia 50 ya nchi yetu kutoka asilimia 16 ya sasa.

Aidha, uongezaji thamani madini ni eneo lingine la kipaumbele kwa Tanzania ili kuhamasisha ujenzi wa viwanda vya kuchenjua, kuyeyusha na kuongeza thamani madini na kuhakikisha shughuli hizo zote zinafanyika nchini ili kuongeza thamani ya madini yanayozalishwa nchini, kuongeza mapato yatokanayo na shughuli za madini na kupanua wigo wa ajira.

Tanzania katika mkutano huo imejikita katika kuendelea kutangaza na kuhamasisha fursa za kiuwekezaji zilizopo katika sekta ya madini nchini. Fursa zimejikita katika utafutaji, uchimbaji, uchenjuaji na uongezaji thamani madini.

Sambamba na dhamira ya Serikali ya kuboresha mazingira ya biashara ya madini zikiwemo Sheria na Kanuni, zinazosimamia shughuli za madini nchini, uendelezaji wa rasilimali watu ili kuwa na usimamizi madhubuti wa sekta ya madini na kuhamasisha ubia wenye manufaa kwa pande zote.

Katika mkutano huo, Tanzania imepata nafasi ya kuwa na siku maalum ya kukutana na wadau mbalimbali ambapo itapata wasaa wa kutoa wasilisho na kutangaza fursa zake za uwekezaji na biashara ya madini zilizopo nchini.

Hivyo, mkutano huo ni fursa adhimu ya kuifanya Sekta ya Madini kuendelea kuchangia katika kukuza uchumi wa nchi yetu kutokana na rasilimali madini zilizopo.

Mkutano wa Indaba ni moja ya mikutano mikubwa ambayo huwakutanisha wawekezaji wapatao 900, taasisi za kisekta 40 na watendaji wakuu wa kampuni kubwa 1000.

Ushiriki wa Tanzania katika mkutano huo unadhaminiwa na kampuni chini ya mwanvuli wa Chemba ya Migodi ikihusisha kampuni za Barrick Gold, Anglo Gold Ashanti, Tembo Nickel, Shanta Gold, Mantra Tanzania, TRX Gold, Petra Diamond, Orica, City Engineering na AUMS.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news