DAR ES SALAAM-Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu na National Agency for Administrative City Construction (NAACC) Heerim Architects and Planners kutoka Korea Kusini wamesaini Hati za Makubaliano (MoU) kwa ajili ya kuliendeleza Jiji la Dodoma.
Hafla hiyo ambayo imewakutanisha watumishi na viongozi mbalimbali waaandamizi kutoka hapa nchini na Korea Kusini imefanyika leo Januari 26,2024 jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera,Bunge na Uratibu), Mheshimiwa Jenista Mhagama amesema kuwa,hatua hiyo inatokana na utayari wa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kuliendeleza Jiji la Dodoma.
"Utiaji saini wa makubaliano haya unatokana na utayari wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuliendeleza na kulipendezesha Jiji la Dodoma ambapo ndiyo Makao Makuu ya Nchi yetu.
"Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa maono yake na tunatarajia kuona maendeleo makubwa zaidi katika nyaza za uchumi, jamii na siasa katika kipindi cha utawala wake kama Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania."
Amesema, Tanzania na Korea wamedumisha uhusiano wa kidiplomasia na ushirikiano katika nyanja nyingi zenye manufaa kwa zaidi ya miaka 30.
Katika muda wote wa ushirikiano huo, Mheshimiwa Mhagama amesema, nchi zote mbili zimeendelea kunufaika kiuchumi na kijamii.
"Mfano, hadi sasa Korea Kusini imeikopesha Tanzania zaidi ya Dola za Marekani milioni 450 ambazo zimetumika kuendeleza miradi mikubwa ya kimkakati kwa maendeleo ya nchi na watu wetu.
"Kusainiwa kwa hati za makubaliano leo kutaweka msingi imara wa biashara na uwekezaji kati ya nchi zetu mbili huku tukitarajia miradi mingi zaidi kutekelezwa katika nchi yetu hususani jijini Dodoma ambako ndiko yalipo makao makuu ya nchi."
Pia amesema, ushirikiano uliopo kati ya nchi zetu mbili umepelekea utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimkakati likiwemo daraja maarufu la Tanzanite ambalo lilijengwa kwa ufadhili wa Serikali ya Korea Kusini kupitia Mfuko wa Ushirikiano wa Maendeleo ya Kiuchumi (Economic Development Cooperation Fund – EDCF).
Daraja hilo ni miongoni mwa miundombinu inayovutia zaidi Dar es Salaam na limekuwa alama ya urafiki na ushirikiano wetu na Korea Kusini.
"Uhusiano wetu umedhihirishwa pia na ziara za viongozi wa ngazi ya juu katika Mataifa yetu haya mawili.
"Moja ya ziara hizo maalum ilifanywa Oktoba 2022 na Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye alifanya ziara ya kikazi nchini Korea Kusini."
Akiwa Korea Kusini, Waziri Mhagama amesema,Waziri Mkuu aliitembelea National Agency for Administrative City Construction, taasisi hii ni Wakala wa Kitaifa nchini Korea Kusini inayosimamia na kuendeleza ujenzi wa Jiji la Sejong, nchini humo.
"Kimsingi, Jiji la Sejong limejengwa kwa mandhari nzuri na ya kuvutia sana.
"Mwonekano wake wa kuvutia ulimfanya Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa niaba ya Serikali ya Tanzania kumkaribisha Mtendaji Mkuu wa taasisi hii nchini Tanzania ili kubadilishana uzoefu na viongozi wa taasisi zinazofanana na hizi hapa kwetu Tanzania.
"Kufuatia mwaliko huo, timu za Wataalamu kutoka Serikali ya Korea Kusini na Tanzania zilianza mara moja kuandaa mipango na mikakati ya awali ili kufikia lengo hilo.
"Hatimaye leo Mtendaji Mkuu wa taasisi hii ya usimamizi wa ujenzi wa Jiji yuko hapa kwa niaba ya Jamhuri ya Korea Kusini na sote tunashuhudia utiaji saini wa Hati za Makubaliano, kuashiria mwanzo wa ushirikiano wetu katika maendeleo na upendezeshaji wa Jiji la Dodoma."
Hati za Makubaliano zilizosainiwa leo,Waziri Mhagama amesema, zinaonesha wazi faida ambazo kila upande itafaidika nazo.
Kwa upande wetu, ushirikiano huu utatunufaisha teknolojia ya kisasa ya usanifu na ujenzi wa majengo na miundombinu mingine itakayopendezesha mji wetu mkuu.
"Pia tutapata fursa mpya za ushirikiano na makampuni ambayo yana uzoefu mkubwa wa usanifu na ujenzi hususan wa majengo katika miji na majiji makubwa."
Amesema,maendeleo ya Jiji la Dodoma yanahitaji uwekezaji mkubwa katika majengo, maeneo ya mapumziko, mazingira, miundombinu ya mawasiliano na maeneo mengine ya kuvutia.
"Lengo hili litafikiwa kwa ufanisi endapo Serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi ili kufikia maendeleo haya.
"Kwa kuzingatia hilo, nitoe wito kwa wawekezaji katika nyanja zote, wanaume kwa wanawake kuwekeza jijini Dodoma ili kuuendeleza na kuupendezesha mji wetu mkuu.
"Kwa mfano, makampuni ya Korea yanashiriki kikamilifu katika miradi ya kimkakati ya ujenzi wa Reli ya Standard Gauge (SGR) pamoja ujenzi wa meli katika Ziwa Victoria.
"Tunatumai kampuni nyingi zaidi za Korea Kusini zitaendelea kufanya kazi na kuwekeza nchini Tanzania, hasa jijini Dodoma kwa kuwa bado tuna kazi kubwa ya kutekeleza kwa ajili ya kuendeleza makao makuu ya nchi yetu,"amefafanua Waziri Mhagama.