NA FRESHA KINASA
CHEMBA ya Biashara Viwanda na Kilimo (TCCIA) nchini imesema kuwa, imejidhatiti kuhakikisha inaunga mkono juhudi za Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kukuza maendeleo na kuimarisha uchumi wa nchi kwa kuongeza shughuli za kibiashara na uwekezaji ndani na nje ya nchi.
Pia, kukuza ubunifu pamoja na kushirikiana na balozi mbalimbali na mashirika ya Kimataifa kibiashara katika kuleta maendeleo hapa nchini.
Hayo yamebainishwa leo Januari Mosi, 2024 na Makamu wa Rais wa Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo, Boniphace Ndengo kwa niaba ya Rais wa TCCIA, Vincent Minja wakakati akizungumza na waandishi wa habari Mjini Musoma mkoani humo.
Aidha, ametoa salamu za mwaka mpya na kuishukuru Serikali na Watanzania wote kwa umoja na mshikamo ambao wameendelea kuudumisha.
Ndengo amesema kuwa,TCCIA itaendelea kukuza ubunifu na kuwalea wanawake na vijana kibiashara ili watimize ndoto zao na kuwa mbia namba moja wa serikali kupitia utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikiwemo kuhakikisha sekta ya madini, biashara, viwanda.
Sambamba na kilimo vinakuwa na manufaa katika kuchangia maendeleo na uchumi wa taifa kufikia asilimia saba na kuendelea.
Amesema kuwa,Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuweka mazingira mazuri na wezeshi kwa wafanyabisahara, wajasiriamali na wawekezaji kuja kufanya uwekezaji hapa nchini.
Hivyo, TCCIA inapongeza juhudi hizo na kuahidi ushirikiano pamoja na kuendelea kuzalisha biashara mpya na fursa ambazo zitaleta tija na kuzidi kuitangaza Nchi kikanda na Kimataifa.
"Yapo mataifa kama China, India, Canada, Marekani na Africa Kusini ambayo yana makampuni mengi ya umma, TCCIA tumekusudia kuwaunganisha Watanzania tuwekeze katika shughuli za makampuni ya umma ili kukuza vipato vya Watanzania na pia kuchangia katika maendeleo ya nchi na kumuunga mkono Mheshimiwa Rais ambaye ametoa dira madhubuti ambayo ni msingi katika kukuza na kuchochea maendeleo ya nchi yetu," amesema Ndengo.
Aidha,ameongeza kuwa, chemba hiyo itaendelea kuimarisha mahusiano na wadau mbalimbali wa maendeleo na pia amewaomba wanachama wa TCCIA kuendelea kushirikiana na uongozi wa chemba uliopo madarakani pamoja na kulipa ada ambazo zinasaidia utekelezaji wa majukumu mbalimbali.
Pia, amewahimiza wanachama wa TCCIA na wafanyabisahara wote kwa ujumla kupunguza mivutano na migogoro na Serikali pamoja na kuzingatia kulipa kodi za serikali,kwani zinaisaidia kutekeleza miradi ya maendeleo kwa wananchi.
"TCCIA tutaendelea kuwasemea wafanyabisahara na wajasiriamali wote kupitia vikao mbalimbali ambavyo pia kwa bahati nzuri Mheshimiwa Rais ni Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Biashara.
"Lengo ni kuona sekta binafsi mchango wake katika maendeleo unaonekana na kama kuna changamoto zinatatuliwa na fursa zinawanufaisha wafanyabisahara na Watanzania wote,"amesema Ndengo.