DAR ES SALAAM-Idara ya Udhibiti ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), imefanya mafunzo ya ukaguzi wa mbolea kwa watumishi ili kuwajengea uwezo na kuongeza uelewa wa shughuli za ukaguzi ikiwa ni jukumu la msingi la mamlaka.
Mafunzo hayo yamefanyika katika ukumbi wa mikutano wa mamlaka mwishoni mwa wiki yakiwa na mwitikio mzuri kufuatia maswali mbalimbali yaliyokuwa yakiibuliwa na washiriki wa mafunzo hayo walioonesha utayari wa kujifunza, kuelewa na kulifurahia somo.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Idara ya Udhibiti, Happiness Mbelle, Meneja wa Sehemu ya Ukaguzi,Dkt. Asheri Kalala alisema, mafunzo hayo yamelenga katika kuwajengea uwezo wafanyakazi wote wa Mamlaka juu ya namna ukaguzi wa mbolea unafanyika bandarini au bandari kavu.
Dkt.Asheri ameongeza kuwa, watumishi wakiwa na uelewa na masuala ya ukaguzi itapelekea kupunguza uwezekano wa kuathiri sampuli za mbolea zinazochukuliwa bandarini kwa ajili ya kupelekwa maabara ili kupima na kujiridhisha na ubora wa mbolea kabla ya kuwafikia walaji au wakulima.
Amesema, kutokuwa na elimu ya uhifadhi wa sampuli za mbolea kunaweza kusababisha uhifadhi mbaya na hivyo kupelekea matokeo hasi ya ubora wa mbolea tofauti na aliyojiridhisha mfanyabiashara na kusababishia uchelewevu wa kuuzwa bidhaa hiyo na mkulima kutokupata tija kwenye kilimo kutokana na kutokutumia mbolea kwa wakati
Aidha, Dkt. Kalala alisema kuwa, ukaguzi wa mbolea ni takwa la kisheria lenye lengo la kuhakikisha mbolea inayoenda kwa wakulima inakidhi viwango kulingana na taarifa zinazoletwa Kwa mamlaka na inaendana na taarifa za mbolea hizo kama zilivyowasilishwa na mtengenezaji au mfanyabiashara wa mbolea alivyoonyesha kwenye nyaraka za kuomba kibali cha kuingiza mbolea nchini.
Akizungumza mara baada ya mafunzo hayo, Mtunza Kumbukumbu Mwandamizi, Sikujua Kassim alisema, mafunzo hayo yamewaongezea uelewa wa namna ya kutuza sampuli za mbolea zinazopokelewa ofisini kwao kabla ya kuzipeleka maabara.
Mafunzo hayo yalihusisha mada za muonekano wa nje wa mbolea, Ukaguzi wa kitaalam (professional Judgement), hatua za kufuata wakati wa kufanya ukaguzi bandarini Kanuni na mbinu za kufanya ukaguzi wa mbolea bandarini na bandari kavu (Port and ICDs).