ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali ya Awamu ya Nane imedhamiria kuimarisha miundombinu ya barabara Mijini na Vijijini Unguja na Pemba.
Amesema malengo ya Serikali ni kuziimarisha barabara zilizopo na kujenga mpya katika maeneo ambako barabara hazijafika kwa kuimarisha mtandao wa barabara nchini.
Rais Dkt.Mwinyi amesema hayo Januari 4, 2024 alipofungua Barabara ya Kijangwani-Birikau, Wilaya ya Chakechake Mkoa wa Kusini Pemba katika shamrashamra za Miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Aidha, Rais Dkt.Mwinyi ameeleza kuwa Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi imeingia mikataba mbalimbali na wakandarasi kutoka nchi tofauti kuzijenga barabara za Mijini na Vijijini.
Vilevile Serikali imengia mkataba na kampuni ya Iris ya Uturuki wa ujenzi wa barabara za ndani urefu wa kilomita 275 Unguja na Pemba ambazo ujenzi unaendelea, pia kampuni ya Propav kwa ujenzi wa barabara kuu urefu kilomita 130 zinazojumuisha barabara ya Chake hadi Mkoani, Tunguu hadi Makunduchi, Fumba hadi Kisauni tayari mkataba umesainiwa hatua itakayoleta mapinduzi makubwa katika sekta ya barabara.
Pia, tayari Serikali imetiliana mkataba na kampuni ya CECC kwa ajili ya ujenzi wa barabara zote za Mjini Unguja zenye urefu wa kilomita 100.
Halikadhalika Rais Dkt.Mwinyi ameeleza kuwa Serikali ya awamu ya nane inajenga kilomita 800 za barabara kati ya Kilomita 1300 za mtandao za barabara zote Zanzibar.
Kwa upande mwingine Rais Dkt.Mwinyi ameishukuru Taasisi ya Milele Foundation kwa uzalendo wa kushirikiana na Serikali kukamilika kwa barabara ya Kijangwani Birikau.