NA LWAGA MWAMBANDE
MARA zote Serikali imeendelea kutoa kipaumbele katika huduma za afya zenye ubora na zinazowafikia wananchi wote ili kuboresha afya zao.
Aidha,Serikali inatambua umuhimu wa afya bora kwa wananchi wake, kwani afya bora ni raslimali muhimu kwa maendeleo.
Ni wazi kuwa, maendeleo ya Taifa letu la Tanzania yataletwa na wananchi wenye afya na wenye uwezo wa kuzalisha mali.
Katika kuhakikisha kuwa wananchi wana afya bora, Serikali imeendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kutoa huduma za afya kwa kuzingatia sera na miongozo iliyopo.
Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasisitiza kuwa, bima ya afya kwa kila Mtanzania ni nguzo muhimu katika Sekta ya Afya, hivyo ili kuhakikisha bima inatumika kikamilifu uhakiki ni muhimu kuepuka udanganyifu. Endelea;
1.Ni Bima yetu ya afya, inayotuhudumia,
Endapo ni mbaya afya, sipitali twafikia,
Lengo irudie afya, tuweze kufurahia,
Uhakiki ni muhimu, kutoa udanganyifu.
2.Kweli ukiwa mgonjwa, vigumu kusubiria,
Waona nguvu wavunjwa, yako wakifwatilia,
Lengo kukwepa kupunjwa, huduma wanodandia,
Uhakiki ni muhimu, kutoa udanganyifu.
3.Katika jamii yetu, haya yametufikia,
Siyo wanachama wetu, bima wanaitumia,
Mapato yabaki butu, Serikali yaumia,
Uhakiki ni muhimu, kutoa udanganyifu.
4.Bila ya udanganyifu, wa huduma kutumia,
Tusingetaka wasifu, wale tunahudumia,
Uongo ndio wakifu, takwimu zatufikia,
Uhakiki ni muhimu, kutoa udanganyifu.
5.Wewe na wako ubini, bima mejisajilia,
Rafiki yako fulani, kadi unampatia,
Huduma sipitalini, bure anajipatia,
Uhakiki ni muhimu, kutoa udanganyifu.
6. Kweli kwenye kuhakiki, huduma weza kawia,
Hili na tuliafiki, ni hatua twapitia,
Tuondoe unafiki, Bima yetu kuibia,
Uhakiki ni muhimu, kutoa udanganyifu.
7. Twaenda bima kwa wote, sote tunafurahia,
Lakini muhimu wote, miiko kuzingatia,
Wizi wa aina zote, tusiweze kusikia,
Uhakiki ni muhimu, kutoa udanganyifu.
8.Bima ya Afya Shirika, zidi kututumikia,
Mipangilio hakika, tuweze kufurahia,
Sipitali tukifika, tuweze kufurahia,
Uhakiki ni muhimu, kutoa udanganyifu.
9.Nasi sote wanachama, bima tunaotumia,
Hebu sote tuwe wema, tuache kudanganyia,
Huduma tupate vema, bila kulalamikia,
Uhakiki ni muhimu, kutoa udanganyifu.
10.Tusotaka kusikia, ni wizi ukazidia,
Kwamba bima twatumia, zisizo halali njia,
Na hapo tutagumia, na lawama kuzidia,
Uhakiki ni muhimu, kutoa udanganyifu.
Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602