ZANZIBAR-Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar,Mhe.Lela Muhammed Mussa amesema, mafanikio makubwa ya ufaulu katika Skuli ya Ng’ombeni A yanatokana na ushirikiano wa dhati kati ya walimu, wazazi na wanafunzi.
Waziri Lela ameyasema hayo katika Ukumbi wa Umoja ni Nguvu Wilaya ya Mkoani, Mkoa wa Kusini Pemba katika hafla ya kuwapongeza wanafunzi wa Skuli ya Ng’ombeni A kufuatia kuogoza kwa ufaulu kitaifa katika matokeo ya mitihani ya darasa la saba.
Amesema,ushirikiano wa pamoja kati ya walimu, wazazi na wanafunzi ulipelekea kufanikisha mikakati mbalimbali ikiwemo kambi ya masomo ya ziada ambayo imepelekea idadi ya wanafunzi waliofaulu michepuo kuongezeka.
Aidha, Mhe. Lela amewataka walimu kuongeza jitihada ikiwa ni pamoja na utunzaji wa miundombinu ili kuhakikisha kwamba wanaendelea kushika nafasi hiyo kutokana na matumizi mazuri ya rasilimali walizonazo.
Aidha,Mhe. Lela amesema, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Elimu itaendelea kutatua changamoto mbalimbali ikiwemo uhaba wa vyumba vya kusomea pamoja na uhaba wa walimu ili kuleta maendeleo mazuri katika Sekta ya Elimu.
Naye Afisa Mdhamini Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Mwalimu, Moh’d Nassor Salim amesema, ni furaha kubwa kwa wazazi, walimu na wanafunzi wa Wilaya ya Mkoani kutokana na kuongoza kwa ufaulu kitaifa.
Amesema, mafanikio hayo yamechangiwa na wadau mbalimbali vikiwemo vyombo vya ulinzi na usalama kwa kufanya jitihada kubwa ya kuwafuatilia na kuwarejesha skuli wanafunzi watoro.
Akisoma Risala Maalumu katika hafla hiyo, Mwalimu Mwanajuma Hassan Kaduara amesema, skuli hiyo imefanya vizuri katika matokeo ya mitihani licha ya changamoto mbalimbali zinazoikabili.
Akitaja baadhi ya changamoto hizo, Mwalimu Mwajuma amesema, skuli hiyo ina uhaba wa walimu sambamba na uhaba wa vyumba vya kusomea jambo ambalo linapelekea kufanya kazi katika mazingira magumu.
Skuli ya Ng’ombeni A imeibuka mshindi Kitaifa baada ya kufaulisha wanafunzi 51 wa nichepuo mbalimbali kati ya wanafunzi 157 waliofanya mtihani huo.