NA LWAGA MWAMBANDE
MAISHA kibinadamu ni kipindi cha muda kutoka kuzaliwa mpaka kufa. Katika kipindi hicho yafaa utambue kuwa, unapaswa uishi kwa mipango yako mwenyewe, kwani maisha ni mipango.
Picha na certainlyher
Ndiyo maana unapaswa kutumia vikwazo vilivyopo katika maisha ili kubadilisha maisha yako. Kwani, kufanikiwa katika maisha ni ile hali ya kutoka hali fulani ya maisha kwenda katika hali nyingine ya maendeleo.
Inashauriwa, mara nyingi tusipende kuishi maisha ya kuiga,tuishi maisha yetu wenyewe.Isikilize nafsi yako inataka nini,usifanye kitu au jambo kwa sababu fulani amesema au amefanya.
Fanya na amua mambo wewe kama wewe,acha kuishi kwa maigizo.Unapotaka kubadilisha maisha yako kuwa wewe,mabadiliko ya maisha yako ni wewe mwenyewe. Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anabainisha kuwa, maisha huwa yanatokea siyo ya kusubiria. Endelea;
1.Maisha yanatokea, siyo ya kusubiria,
Na kuishi endelea, malengo yatatimia,
Changamoto zatokea, uache kulialia,
Kama wangoja amani, utasubiria sana.
2.Maisha yanatokea, vurugu zinaingia,
Kuishi twaendelea, huku twajipambania,
Haitapata tokea, kila kitu kutulia,
Kama wangoja amani, utasubiria sana.
3.Changamoto twapokea, zote kwetu zaingia,
Twapambana twasogea, huku tukivumilia,
Hakuna cha kulegea, yetu yapate timia,
Kama wangoja amani, utasubiria sana.
4.Hapa tulipotokea, Mungu hakutuambia,
Kwamba hakutatokea, mambo kutuumizia,
Magumu yayotokea, vema twayachukulia,
Kama wangoja amani, utasubiria sana.
5.Mawimbi yanatokea, kutaka kutufukia,
Nasi tunajitetea, mbinu nyingi twatumia,
Ndivyo tunaendelea, siku mpya zaingia,
Kama wangoja amani, utasubiria sana.
6.Kile kinatukolea, ambacho tunaringia,
Mungu anaendelea, nuru kutuangazia,
Mapigo yanatokea, siku mpya twaingia,
Kama wangoja amani, utasubiria sana.
7.Nyumbu kuwaelezea, pengine itaingia,
Mto Mara huendea, msimu ukiwadia,
Ni wengi wanapotea, ng’ambo wanaisikia,
Kama wangoja amani, utasubiria sana.
8.Wengine huendelea, ng’ambo waweze fikia,
Maisha yaendelea, japo shida zazidia,
Nawe ndugu endelea, nguvu za kwako tumia,
Kama wangoja amani, utasubiria sana.
9.Mema ili kupokea, ulipo sijetulia,
Lazima kuyaendea, uweze jinyakulia,
Miiba ikitokea, songa mbele vumilia,
Kama wangoja amani, utasubiria sana.
10.Vita vinaendelea, ndoa watu waingia,
Hao wanaendelea, watoto wajipatia,
Endapo wangengojea, hilo lisingetimia,
Kama wangoja amani, utasubiria sana.
11.Mkulima egezea, shamba kijiandalia,
Si mtu wa kungojea, hadi mvua kuingia,
Imani imekolea, mvua itamjia,
Kama wangoja amani, utasubiria sana.
Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602