Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania (TAEC) inaendelea kusogeza huduma kwa wananchi ambapo kwa sasa TAEC imekamilisha Ujenzi wa Maabara na Ofisi Zanzibar eneo la Dunga Zuze kwa jumla ya shilingi Bilioni 2.8 zilizogharamiwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan.
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC ),Prof. Lazaro Busagala anakupa ufafanuzi zaidi, endelea katika video hapa chini;
TAEC ni nini?
Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC) iliundwa kwa Sheria ya Nguvu za Atomu Na. 7 ya Mwaka 2003 (Atomic Energy Act No.7 of 2003).Sheria ya Bunge Na. 7(2003) ilifuta Sheria Na.5 ya mwaka 1983 (The Protection from Radiation, No. 5 of 1983) iliyoanzisha Tume ya Taifa ya Mionzi (National Radiation Commission).
Sheria hii imeipa TAEC mamlaka ya kudhibiti matumizi salama ya mionzi nchini ikiwemo kuhamasisha matumizi salama ya teknolojia ya nyuklia nchini.
Ni kutokana na ukweli kwamba, teknolojia ya nyuklia inatumika katika sekta mbalimbali za kiuchumi na kijamii kama vile afya, kilimo, ufugaji, viwanda, maji na utafiti.
TAEC imepewa jukumu la kupima mionzi kutokana na sababu mbalimbali, kwani licha ya kuwa na faida nyingi za mionzi, isipotumika inavyotakiwa ni hatari ikiingia katika mnyororo wa chakula kwa sababu inatoa nishati toka katika kiini cha atomu ambayo haiwezi kuharibiwa kwa aina yoyote ile.
Kwa mujibu wa tume hiyo, viasili vya mionzi vinaweza kuathiri afya ya binadamu na wanyama. Hivyo, sababu kuu za kupima mionzi katika mnyororo wa chakula ni kuhakikisha chakula kinacholiwa na Watanzania hakina mionzi na hivyo kuwa salama kwa matumizi ya kawaida.
Pia ni muhimu kuhakikisha kuwa soko la bidhaa zinazouzwa nje ya nchi zinalindwa ili kuzingatia ubora na viwango vilivyowekwa kulingana na miongozo na taratibu mbalimbali za Serikali.
Miongoni mwa sababu zinazosababisha upimaji wa mionzi ni kutokana na ukweli kuwa, usafirishaji usio rasmi wa vyanzo vya mionzi (illicit trafficking) unaweza kusababisha uchafuzi kwenye vyakula na mazingira.
Sababu nyingine kwa mujibu wa TAEC ni kuwepo kwa mionzi asili kwenye udongo na mazingira yetu kama vile madini ya urani katika maeneo mbalimbali nchini.
Pia kila mmoja wetu anatambua kuwa, ni wajibu wa Serikali kulinda wananchi, hivyo kupitia tume hiyo imechukua hatua za kulinda mnyororo mzima wa chakula ili wananchi wake wawe salama
Sambamba na kulinda soko la bidhaa zetu zinazouzwa nje ya Tanzania hasa wakati huu wa vita ya kiuchumi. Upimaji unatoa uwezekano wa kufuatilia kama kuna shida yoyote ikiewemo kutekeleza takwa la kisheria, kupima mionzi kwenye mnyororo wa bidhaa kama ilivyoahinishwa kwenye Sheria Na. 7 ya Mwaka 2003.
Sheria hii inaendana na matakwa ya Kimataifa ikiwemo Shirika la Afya Duniani (WHO), Shirika la Kilimo na Chakula Duniani (FAO) na Shirika la Nguvu za Atomiki Duniani (IAEA).