NA DIRAMAKINI
MAISHA ni safari ndefu, kuna wakati unaweza kustawi zaidi katika kila nyanja, lakini ikafika mahali ukaporomoka hadi ukajutia kwa nini Mungu amekusahau.
Vijaypat Singhania ambaye alizaliwa Oktoba 4, 1938 huko Kanpur nchini India ni miongoni mwa waliokuwa wafanyabiashara wakubwa zaidi ambao walikuwa na ukwasi wa kushangaza, lakini ukimuona mzee huyo kwa sasa unaweza ukatokwa na machozi.
Singhania alikuwa mkuu wa himaya yote ya Raymond Group. Miongoni mwa makampuni makubwa zaidi nchini India ambayo huzalisha nguo na vitambaa vya kisasa.
Raymond inasifika kwa uzalishaji wa vitambaa vya kisasa kwa ajili ya mashati, suti, nguo za kitani, pamba na nyinginezo ambazo zinasifika zaidi kwa ubora ndani na nje ya India.
Akiwa ndiye mwasisi ambaye alihudumu kama mwenyekiti na mkurugenzi mkuu wa Raymond Group kutoka mwaka 1980 hadi 2000, Singhania wakati huo alikuwa mmoja wa watu tajiri zaidi nchini India.
Lakini mambo yalienda mrama na meza ikapinduliwa. Ni jambo ambalo hauwezi kuamini, lakini ukweli ni kwamba Singhania, ambaye wakati mmoja alikuwa mmoja wa watu tajiri zaidi wa India, sasa anaishi katika nyumba ya kupanga.
Wakati fulani, Vijaypat Singhania alikuwa tajiri zaidi kuliko Mukesh Ambani na majina mengine makubwa ya biashara, kwani walikuwa wachanga sana wakati Singhania alikuwa tayari mmiliki wa Raymond Group.
Kila kitu kilikuwa kikimwendea sawa, lakini mtoto wake alimfukuza nyumbani kwake. Ilianza wakati Singhania alipoandikisha hisa zote za kampuni yake kwa jina la mwanaye, Gautam na kutoka wakati huo, uhusiano kati ya baba na mtoto ulianza kuvunjika.
Wakati fulani ugomvi ulikua sana, ikafikia hatua Gautam kumtimua Vijaypat Singhania kutoka katika nyumba yake mwenyewe, kulingana na mahojiano ambayo Vijaypath Singhania alifanyiwa na Business Today.
Vijaypat, katika mahojiano hayo, pia alisema kwamba mtoto wake Gautam alimnyang'anya kila kitu, na kwamba anaishi kwa pesa kidogo aliyobaki nayo.
“Sina biashara. Alikuwa amekubali kunipa baadhi ya sehemu za kampuni. Lakini bila shaka, kwake kurejea hilo ni mkataba wa sekunde mbili.
"Kwa hivyo sina kitu kingine, nilimpa kila kitu. Kwa makosa nilibakiwa na pesa ambazo leo ninaishi. Vinginevyo ningekuwa njiani.
"Angefurahi kuniona barabarani. Nina uhakika na hilo. Kama aliweza kumtoa mke wake hivi, kumtupa baba yake hivi sijui ni kitu gani,” alisema.
Alisema kwamba wazazi kama yeye wanapaswa kufikiria mara mbili kabla ya kuwapa watoto wao kila kitu.
"Kwa vyovyote vile, toa kile unachotaka. Sikwambii usimpe. Ninasema tu, toa baada ya kuondoka, baada ya kifo chako. Usimpe maishani mwako kwa sababu unaweza kulipa gharama kubwa sana,”Vijaypat Singhania aliongeza.
Wakati huo huo, Vijaypat Singhania mwanzilishi wa Raymond Group na baba wa Mkurugenzi Mtendaji na Mwenyekiti wa kampuni hiyo, Gautam Singhania alizungumza kuhusu mtoto wake huyo ambaye amekuwa akigonga vichwa vya habari tangu alipotangaza kutengana na mkewe, Nawaz Modi Singhania.
Katika mahojiano ya kipekee na Business Today, bosi huyo wa zamani wa Raymond alisema kuwa hataki kuingilia uamuzi uliotolewa na Gautam Singhania na Nawaz Modi Singhania.
Aliweka wazi kuwa anasimama na mkaza mwana (mkwe) wake na atamsaidia na si mtoto wake. Alipoulizwa kama atakuwa tayari kuzungumza na mwanaye iwapo Nawaz Modi Singhania atamkaribia, Vijaypat Singhania alisema, "Jibu langu la kwanza litakuwa ndiyo, ningekuwa tayari kukutana naye.
"Jibu langu la pili ni kwamba kukutana naye (Gautam Singhania) hakuna. maana hatanisikiliza.Na nikisema jambo asilolipenda, anaweza kunifokea, anaweza kunitusi. Anafanya mambo ya aina hii. Kwa hiyo, labda ningejaribu kujiweka pembeni kadiri niwezavyo," aliongeza. (BT)