DAR ES SALAAM-Katika kuendelea kuboresha huduma za Afya, Serikali kupitia Wizara ya Afya imeongeza vitanda 1,000 vya kuhudumia wagonjwa mahututi (ICU) kwa mwaka 2023 kutoka vitanda 528 kwa mwaka 2022.
Waziri Ummy amesema hayo wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika katika ofisi ndogo ya Wizara ya Afya jijini Dar es salaam akitoa taarifa ya hali ya utoaji huduma za afya nchini kwa mwaka 2023.
“Ongezeko hili la vitanda vya kuhudumia wagonjwa wa ICU linaboresha huduma lakini kubwa linapunguza vifo ambavyo vingeweza kutokea ndani ya hospitali ambavyo vimeweza kuzuilika kwa asilimia 20 hadi asilimia 30,” amesema Waziri Ummy.
Waziri Ummy ametolea mfano kwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa ambapo amesema kulikuwa na vitanda 8 kwa Mwaka 2021, kwa Mwaka 2023 vitanda hivyo vimeongezeka kufikia 20 kwa hivyo kuwezesha hospitali hiyo kuhudumia wangonjwa mahututi 20 kwa mara moja.