ZANZIBAR-Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Mapindizi Zanzibar inayoongozwa na Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi imeanza utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa vyuo vitano vya kisasa vya mafunzo ya Amali kote nchini.
Amesema ujenzi wa vyuo hivyo utakamilisha shabaha ya Serikali kuwa na Chuo cha Amali kikubwa na cha kisasa katika kila wilaya, huku lengo likiwa ni kuhakikisha vijana wote wanapata ujuzi na utaalamu utakaowasaidia kukabiliana na ushindani wa soko la ajira ndani na nje ya nchi hasa katika fani za Uchumi wa Buluu.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo, Jumatano, Januari 10, baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa Skuli ya Muungano iliyopo Wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini Magharibi, Zanzibar. Skuli hiyo ambayo itakuwa na madarasa 41 itagharimu shilingi bilioni 6.1 mpaka kukamilika kwake. Uwekaji huo wa jiwe la msingi ni sehemu ya shamrashamra za maadhimisho ya miaka 60 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
Pia, Mheshimiwa Majaliwa amemtaka mkandarasi anayejenga mradi huo ambao ulianza kujengwa Mei 2023 na unatarajiwa kukamilika Aprili, 2024, ahakikishe unakamilika kwa wakati na kwa ubora na viwango vilivyokusudiwa.
“Mwezi Aprili shule hii iwe imekamilika. Tunapoweka malengo ya ujenzi na tukakubalina muda basi lazima ujenzi huo ukamilike kwa wakati.”
“Kipekee ninampongeza sana Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa kazi nzuri anayoifanya katika kuyaendeleza na kutekeleza malengo ya Mapinduzi ya Zanzibar na Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwa vitendo. Rais Mwinyi ni kiongozi mwenye busara, hekima na mchapakazi mwenye kuwatumikia wananchi wake kwa kuwaletea maendeleo wanayoyataka kwa kasi kubwa.”
Mheshimiwa Majaliwa amesema kila mwananchi ni shahidi wa mabadiliko makubwa ya kimaendeleo yaliyofanyika Zanzibar katika kipindi kifupi kwani mbali na maboresho hayo katika sekta mbalimbali ikiwemo ya elimu, Mheshimiwa Rais Dkt. Mwinyi ameendeleza umoja, mshikamano, amani na utulivu Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.
Waziri Mkuu amesema hali hiyo imekuwa kichocheo katika kutekeleza shughuli mbalimbali ya kuwaletea wananchi Maendeleo. Mwenyezi Mungu amzidishie afya njema hekima na busara katika kuwatumikia zaidi wananchi. Haya ndio malengo hasa ya mapinduzi.
Kwa upande wake, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Lela Muhamed Mussa (Mb.) ametumia fursa hiyo kutaja baadhi ya mafanikio yaliyopatikana upande wa sekta ya elimu katika kipindi cha miaka 60 ya Mapinduzi kuwa ni pamoja kuongezeka kwa Bajeti ya sekta ya elimu kutoka shilingi bilioni 265.5 mwaka 2021/2022 hadi kufikia shilingi bilioni 457.2 katika mwaka 2022/2023 sawa na ongezeko la asilimia 72.2.
Amesema kiwango hiko cha bajeti katika historia ya Zanzibar ni kielelezo cha dhamira ya Serikali katika kuendeleza Sekta ya Elimu, ambapo kwa sasa imejipanga kujenga shule 25 za ghorofa katika maeneo mbalimbali ya Unguja na Pemba kwa mwaka wa fedha wa 2023/2024; ikiwemo shule hiyo ya ghorofa tatu (G+3) ya Muungano.