SINGIDA-Vijana mkoani Singida wameanza operesheni maalum ambayo wamesema inalenga kukomesha vitendo vya kishirikina ambavyo vimeendelea kuacha maumivu katika jamii mbalimbali.
Kwa nyakati tofauti vijana hao wakiwa maeneo ya Itigi mkoani humo wamesema, vitendo vya kichawi ambavyo vimekithiri katika maeneo mbalimbali mkoani humo vimekuwa kikwazo.
"Tunafanya msako wa watu wote ambao wanajihusisha na ramli chonganishi na vitendo vya uchawi kwa ujumla.
"Sisi,vijana tukishakamilisha uchunguzi wetu tutavishirikisha vyombo vya ulinzi na usalama ili waweze kuwachukua wahusika wote ambao wanasababisha mifarakano katika jamii na aibu kwa mkoa wetu wa Singida,"amesema mmoja wa vijana hao Hassan Idd kutoka Ikungi mkoani humo.
Wamesema kuwa, operesheni hiyo inafanyika ili kupunguza maafa ambayo yanaweza kutokea ikiwemo baadhi ya vijana kuamua kujichukulia sheria mikononi na kuwadhibiti watu hao ambao wanahisiwa ni washirikina.
"Ushirikina si sifa njema kwa jamii au mkoa wetu, hivyo sisi badala ya kuwaadhisha wachawi hao tunawafichua hadharani na tutawakabidhi mbele ya vyombo vya sheria,"amesema Suleiman mkazi wa Itigi..