Walioonesha ujuzi wa mapishi Zanzibar wazawadiwa, Waziri Pembe atoa wito

ZANZIBAR-Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Mhe. Riziki Pembe Juma amewashauri wajasiriamali nchini kuendelea kutumia ubunifu wao wa kupika vyakula mbalimbali kwa ajili ya biashara zao za mama ntilie ili waweze kujikwamua na umaskini.
Kauli hiyo ameitoa wakati akizungumza na wajasiriamali katika Uwanja wa Urafiki uliopo Jimbo la Shaurimoyo, Unguja katika mashindano ya mapishi ikiwa ni shamrashamra za miaka 60 ya Mapainduzi ya Zanzibar.

Mhe.Riziki amesema, katika kazi yoyote ile inahitaji ubunifu, hivyo ni vyema mama ntilie wawe wabunifu katika mapishi mbalimbali kabla ya biashara ya chakula, kwani hatua hiyo itasaidia kuongeza kipato na kujikwamua dhidi ya umaskini.

Waziri Pembe amewataka wajasiriamali hao kuitumia fursa ya mikopo iliyopo ikiwa ni juhudi ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi ya kuwawekea mazingira wezeshi wajasiriamali kwa nia ya kufikia malengo waliyojiwekea.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Riziki Pembe Juma akimkabidhi mshindi wa kwanza katika mashindano ya mapishi ya chakula (mama ntilie) fedha tasilimu shilingi laki tano, mashindano hayo yamefanyika leo katika Jimbo la Shauri Moyo, Unguja, ikiwa ni shamrashamra za miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Aidha, amesema Oryx Gas na Azania Group wameamua kwa makusudi kuwasaidia wajasiriamali ili kuhakikisha wajasiriamali wote nchini wanafanikiwa na wanakuwa mfano wa kuigwa katika kutoa huduma bora za vyakula popote nchini.

Naye Mwakilishi wa Jimbo la Shaurimoyo ambae pia ni Waziri wa nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi Mhe.Hamza Hassan Juma, amesifu juhudi zinazofanywa na wajasiriamali wa Jimbo la Shaurimoyo kwa kuonesha ubunifu mkubwa wa vyakula mbalimbali ambao utawasaidia kutambulika kitaifa na kimataifa.

Kwa upande wake Mwakilishi kutoka Oryx Gas, Bi.Anjela Bitungwa amesema, wameamua kuwapelekea nishati safi ya kupikia kwa lengo la kulinda mazingira pamoja na afya kwa wajasiriamali wa Jimbo la Shaurimoyo.

Lengo amesema ni ili kuwaepusha na madhara ya kutumia kuni na mkaa na kuahidi kuendelea kuratibu kwa kutoa mitungi ya gesi 200 yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 25.
Naye msimamizi wa biashara kutoka Azania Group, Bw.Joel Laiser amesifu hatua ya maendeleo iliyofikiwa hivi sasa chini ya Rais Dkt.Mwinyi katika kuelekea miaka 60 ya Mapinduzi matukufu ya Zanzibar.

Ameeleza kuwa,Azania Group itaendelea kushirikiana na viongozi wa Zanzibar kwa kuwawezesha wajasiriamali kwa kuwapatia nyenzo zote zinazozalishwa katika kampuni hiyo ili kuwasaidia wajasiriamali hao.

Washindi watatu wamepatikana na kupatiwa zawadi ambapo mshindi wa kwanza katika mashindano ya mapishi ya miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar amezawadiwa shilingi laki tano,mchele,unga wa sembe,unga wa ngano kilo 50 kila mmoja,sukari na mafuta lita 20.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news