Wanaume siyo watu?

NA LWAGA MWAMBANDE

REJEA Biblia Takatifu katika kitabu cha 1 Wakorintho 11:8-12..."Kwa maana mwanaume hakutoka kwa mwanamke, bali mwanamke alitoka kwa mwanaume.
"Wala mwanaume hakuumbwa kwa ajili ya mwanamke, bali mwanamke kwa ajili ya mwanaume.Kwa sababu hii na kwa sababu ya malaika, inampasa mwanamke awe na ishara ya mamlaka juu yake.

"Lakini katika Bwana, mwanamke hajitegemei pasipo mwanaume na mwanaume hajitegemei pasipo mwanamke. Kama vile mwanamke alivyoumbwa kutoka kwa mwanaume, vivyo hivyo mwanaume huzaliwa na mwanamke. Lakini vitu vyote vyatoka kwa Mungu."

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasisitiza kuwa,licha ya upekee wa mwanaume ambao unaelezwa katika Biblia, lakini bado katika dunia ya leo ni wazi kuwa, wanaume wanaonekana siyo watu, kwani dunia hii si yao. Endelea;

1. Wanaume siyo watu, hata wanapouawa,
Wanawake ndiyo watu, si vizuri kuuawa,
Na watoto ndio watu, hawapaswi kuuawa,
Wanaume siyo watu, dunia hii si yao.

2. Vita vingi duniani, watu wengi huuawa,
Waume wapigwe chini, kawaida kuuawa,
Watu wanasema nini, wengi wetu twaelewa,
Wanaume siyo watu, dunia hii si yao.

3.Kote kuliko na vita, wapo wanaotetewa,
Ila wanaume hata, hao watajielewa,
Wauawe kuwafuta, kwa dunia kama kawa,
Wanaume siyo watu, dunia hii si yao.

4.Mapigano kule Kongo, wanawake watetewa,
Na watu wana usongo, watoto wakiuawa,
Kwa wanaume ni chongo, hata wakifagiliwa,
Wanaume siyo watu, dunia hii si yao.

5.Sudani wanapigana, vifo vinahesabiwa,
Watu wajadiliana, wanawake kuuawa,
Tena wanashituana, watoto wanauawa,
Wanaume siyo watu, dunia hii si yao.

6.Sasa Gaza shida kubwa, watu wanaouawa,
Kweli maafa makubwa, na wengi wanaonewa,
Lakini kelele kubwa, nani wanaoliliwa?
Wanaume siyo watu, dunia hii si yao.

7.Waliliwa wanawake, ambao wanauawa,
Na watoto hao peke, ambao wafagiliwa,
Wanaume wako peke, msala wameachiwa,
Wanaume siyo watu, dunia hii si yao.

8.Kwani nani anajali, waume wakiuawa,
Asikitikae kweli, kwamba wanafanyiziwa,
Hao waishie mbali, hatutaki kuambiwa,
Wanaume siyo watu, dunia hii si yao.

9.Acha waume waishe, jinsi wanafagiliwa,
Dunia hii wapishe, hao wazidi zomewa,
Na kesho yetu itishe, waume tukiishiwa,
Wanaume siyo watu, dunia hii si yao.

10.Waume pia ni watu, ni vema wakaenziwa,
Na wao wanao utu, siyo wa kushambuliwa,
Wakiuawa ni watu, ni vema kusikitikiwa,
Wanaume siyo watu, dunia hii si yao.

11.Vita mbaya kwetu sote, vile watu wauawa,
Ni kwa wanadamu wote, uhai kuthaminiwa,
Vema kuwajali wote, pasipo kubaguliwa,
Wanaume siyo watu, dunia hii si yao.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news