ROME-Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb.) amekutana kwa mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya Uhamiaji (International Organisation for Migration-IOM), Bi. Amy Pope jijini Roma, Italia.
Akizungumza katika kikao hicho, Waziri Makamba ameipongeza IOM kwa kazi inazofanya nchini katika masuala ya Uhamiaji na amemuhakikishia Bi. Pope kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itaendelea kufanya kazi na Shirika hilo kwa ukaribu zaidi.
Mhe. Waziri Makamba amesema Shirika hilo limekuwa mstari wa mbele katika kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika masuala ya wakimbizi, majanga ya asili na kwamba ni matumaini yake kuwa Tanzania na IOM zitaendelea kushirikiana kwa manufaa ya pande zote mbili.
Waziri Makamba ameipongeza IOM kwa kuendelea na zoezi la kuwarejesha nyumbani raia wa Ethiopia waliokuwa katika magereza mbalimbali nchini na kuongeza kuwa kitendo hicho kimesaidia Tanzania kukabiliana na changamoto ya msongamano wa watu katika magereza yake.
Kwa upande wake, Bi. Pope ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa jinsi inavyoshirikiana na Shirika la IOM katika kutekeleza majukumu yake na kuahidi kuwa na mpango maalum wa kuendeleza ushirikiano na Serikali ya Tanzania katika kufanikisha majukumu yake. Aliongeza kuwa Shirika hilo litahakikisha kuwa wahamiaji wanapata haki zao za msingi na kuwa katika mazingira salama nchini.