Zanzibar yataja faida uanzishwaji wa Jukwaa la Haki za Watoto

ZANZIBAR-Mkurugenzi Idara ya Mipango, Sera na Utafiti, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto,Bi.Daima Mohamed Mkalimoto amesema, hatua ya uanzishwaji wa Jukwaa la Haki za Watoto kwa wadau wanaoshughulikia maendeleo ya watoto itasaidia kuweka pamoja na kuunganisha shughuli za watoa huduma za watoto.
Mkurugenzi Idara ya Mipango Sera na Utafiti, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto,Bi.Daima Mohamed Mkalimoto akifungua mkutano wa wadau wanaoshughulikia masuala ya Wanawake na Watoto kutoka taasisi za umma, binafsi na Washirika wa Maendeleo katika ukumbi wa UN Women Kinazini.
Amesema hayo katika ukumbi wa UN Women wakati akifungua mkutano wa wadau wanaoshughulikia masuala ya watoto kutoka taasisi za umma, binafsi na washirika wa maendeleo, ambapo mkutano huo ulilenga uanzishwaji wa Jukwaa la Haki za Watoto Zanzibar.

Bi.Daima amesema, hatua hiyo itasaidia kuwaweka pamoja wadau hao katika uratibu wa utekelezaji wa shughuli zinazogusa maendeleo ya watoto nchini.

Hivyo amewaomba wadau hao kutoa maoni yao ili yafanyiwe kazi na kuingizwa katika mapendekezo ya kuanzishwa kwa jukwaa hilo.

“Kuna umuhimu wa uratibu na usimamizi wa pamoja wa uanzishwaji wa jukwaa la haki ya watoto ili kuweza kutoa huduma bora za watoto katika mazingira na hali tofauti,” amesema Bi.Daima.
Akiwasilisha mapendekezo ya kuanzishwa kwa Jukwaa la Haki ya Watoto kwa wadau wanaoshughulikia Maendeleo ya watoto Zanzibar, Mshauri elekezi kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Watoto (UNICEF) na Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu Huria Tanzania,Dkt.Ladislaus Batinoluho ameipongeza Serikali ya Zanzibar kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa hatua nzuri iliyofikia kutokana na kazi kubwa wanayoifanya katika masuala mazima ya maendeleo ya watoto nchini.

Amesema,pamoja na mafanikio hayo, bado watoto wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo utumikishwaji kwa watoto, kudhalilishwa na kubakwa, hivyo wazo la UNICEF la kuanzishwa jukwaa hilo litasaidia kuleta nguvu za pamoja katika kumkomboa mtoto.
Nao washiriki wa mkutano huo, wameshauri kuanza taratibu za kuanzishwa jukwaa hilo ni vyema kuwashirikisha wadau na taasisi zote zinazoshughulikia watoto ikiwemo Wizara ya Elimu, Wizara ya Afya na nyinginezo ili kufikia malengo ya kuanzishwa kwa jukwaa hilo la haki za watoto Zanzibar.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news