BAMAKO-Rais wa Shirikisho la Sanaa za Ufundi Tanzania, Bw. Adrian Nyangamalle ameteuliwa kuwa mwakilishi mkazi wa Kanda ya Afrika Mashariki wa Arterial Network akiongoza nchi za Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Sudani Kusini na Seychelles.
Kwa uteuzi huo uliyofanyika Bamako nchini Mali, Nyangamalle anakuwa mtanzania wa kwanza kushika nafasi hiyo tangu kuundwa shirika hilo.
"Hii ni mara ya kwanza kwa Tanzania kushika nafasi hii kubwa katika umoja huu wa wasanii Afrika iliyokuwa inashikiriwa na Bi. Collen Orishaba wa Uganda.
"Kwa nafasi hii Nyangamalle anakuwa mjumbe wa Kamati Kuu ya Utendaji yenye wajumbe watano barani Afrika.
"Wengine ni Alassane Babylas Ndiaye (Senegali) Kanda ya Magharibi, Rais Stephanie Kafunde (Zimbabwe) Kanda ya Kusini, Makamu wa Rais Manasse Ndoua Nguinambaye (Chad) Kanda ya Kati, Mjumbe; na Cheich Aidara (Morocco) Kanda ya Kaskasini, Mjumbe," ilieleza taarifa hiyo.
Arterial Network ni mtandao unaounganisha wasanii, wanaharakati wa kitamaduni, wajasiriamali, wafanyabiashara, NGOs na taasisi zinaofanya kazi katika sekta za ubunifu na kitamaduni barani Afrika.
Imeanzishwa Machi 2007 nchini Senegal ni shirika lenye msingi wa wanachama, lisilo la faida.
Mtandao huu kiungo cha wasanii Afrika unafanya kazi katika bara zima bila kujali mipaka ya lugha na unaongozwa na Kamati ya Utendaji iliyochaguliwa na ambayo inawakilisha kanda zote tano za bara la hili.
Maeneo matano ya msingi ya Mtandao huu ni Uzengezi, ushawishi na utetezi; Kujenga uwezo; Ufikiaji wa soko; Usimamizi wa maarifa na usambazaji wa habari; kwa miaka kadhaa wasanii na baadhi ya taasisi za Tanzania zimenufaika na mtandao huu.
Amesema, Arterial Network inatambuliwa na Umoja wa Afrika (AU) kama chombo unganishi cha wadau wa sanaa na utamaduni barani humu ambapo kwa sasa Makao Makuu shirika hili yapo Jijini Bamako nchini Mali.
Mara baada ya kupokea uteuzi, Bw Nyangamalle ametoa shukrani kwa wadau wa sanaa barani afrika na Tanzania kwa kuwezesha kupata nafasi hiyo.
“Namshuuru Mwenyezi Mungu kwa baraka zake, namshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuifungua na kuiunganisha nchi na kufanya watanzania tunga’are kimataifa, niwashurukuru watanzania wote kwa sapoti.
"Ahadi yangu ni kwamba nitatumia nafasi hii kuunganisha nchi, kanda na Afrika kwa ujumla kupitia Sanaa na Utamaduni; na wakati wote nitakuwa balozi mzuri wa taifa langu,” alisema Nyangamalle ambaye kwa sasa yuko nchini India kikazi.
Aidha, ametoa wito kwa wasanii kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kuendelea kupeperusha bendera ya Tanzania kimataifa.
Nalo Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) kupitia ukurasa wake wa Instagram limempongeza Nyangamalle kwa uteuzi huo.