BoT ndiyo pekee yenye mamlaka ya kutoa sarafu nchini-Dkt.Lusajo

NA GODFREY NNKO

UWEZO wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) wa kutoa saarafu, kusimamia na kuendesha masoko ya fedha nchini unaiwezesha kwa namna ya kipekee kutekeleza sera za fedha zenye kulenga utulivu wa bei nchini.
Hayo yamebainishwa Februari 14, 2024 jijini Zanzibar na Meneja Msaidizi wa Utafiti kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Dkt.Lusajo Mwankemwa wakati akiwasilisha mada kuhusu majukumu ya BoT katika semina ya siku tatu kwa waandishi wa habari za uchumi nchini.

Amesema, BoT ambayo makao yake makuu yapo jijini Dodoma, pia ina makao makuu ndogo jijini Dar es Salaam na Zanzibar yakiwemo matawi mikoa ya Mwanza, Arusha, Mbeya na Mtwara.

"Sheria ya Benki Kuu ya mwaka 2006 inatamka wazi kuwa, jukumu la msingi la Benki Kuu ni kuandaa na kutekeleza Sera ya Fedha inayolenga kudhibiti mfumuko wa bei.

"Na uwezo wa Benki Kuu wa kutoa sarafu, kusimamia na kuendesha masoko ya fedha nchini,unawezesha Benki Kuu kwa namna ya pekee kutekeleza sera za fedha zenye kulenga utulivu wa bei.

"Kwa kuongeza au kupunguza kiasi cha fedha kilichopo kwenye mzunguko Benki Kuu huweza kupunguza kichocheo cha mfumuko wa bei na kuweka uwiano mzuri kati ya wingi wa sarafu na wingi wa bidhaa au huduma,"amefafanua Dkt.Lusajo

Dkt.Lusajo amesisitiza kuwa, Benki Kuu ndiyo pekee yenye mamlaka ya kutoa sarafu nchini Tanzania kwa lengo la kutosheleza mahitaji ya mzunguko wa fedha katika uchumi bila kusababisha ongezeko la mfumuko wa bei.

Amesema,pia benki inahakikisha usambazaji wa fedha unawafikia watumiaji bila upungufu, kazi ambayo huwa inafanyika kupitia matawi yao ya Mwanza, Arusha, Mbeya, Zanzibar, Dodoma na Mtwara.

Vile vile ameendelea kutoa wito kwa wananchi kuendelea kuzitunza fedha vizuri ili ziwendelee kuwepo katika mzunguko kwa muda mrefu, kwani noti chakavu zimekuwa ziichangia gharama kubwa katika uendeshaji wa benki

"Gharama za uchapishaji, utunzaji, usambazaji na kuharibu noti chakavu ni sehemu kubwa ya gharama ya uendeshaji Benki Kuu."

Katika hatua nyingine. Dkt.Lusajo amesema, utulivu wa bei unawezekana kupatikana endapo kuna uwiano mzuri kati ya Sera ya Fedha na Sera ya Bajeti na nyinginezo za uchumi nchini.

“Sera zote za kitaifa zinapaswa kwenda kwa uwiano, sera ya fedha, peke yake, haiwezi kufanikiwa kufikia utulivu wa bei, hata kama ingekuwa makini kiasi gani.

"Inaweza tu kupunguza mfumuko wa bei kufikia ukomo fulani endapo kutakuwa na shinikizo la mfumuko wa bei linalotokana na sera za mapato na matumizi ya serikali pamoja na sera nyingine za uchumi,"amesisitiza Dkt.Lusajo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news