NJOMBE-Mkurugenzi wa Halmashauri ya mji wa Makambako, Kenneth Haule amezindua kampeni ya utoaji wa chanjo ya surua ambayo itatolewa kwa siku nne kwa watoto wa kuanzia miezi 9 hadi miezi 59 yaani wenye umri chini ya miaka mitano.
Chanjo hiyo imeanza kutolewa Febuari 15 na itatolewa hadi Febuari 18, mwaka huu kwenye vituo vya kutolea huduma za afya vilivyopo mjini Makambako.
Akizindua kampeni hiyo katika kituo cha afya Makambako, Mkurugenzi Kenneth Haule amewataka wazazi na walezi wenye watoto wenye umri chini ya miaka mitano kuhakikisha watoto wao wanapatiwa chanjo hiyo huku akiwataka kuachana na dhana potofu dhidi ya chanjo hiyo.
Mratibu wa Chanjo katika Halmashauri ya Mji wa Makambako, Tindichebwa Mazara amesema,chanjo hiyo itatolewa kwenye vituo vyote vya kutolea huduma za afya na maeneo yenye mkusanyiko wa watu wengi.
Baadhi ya wazazi ambao watoto wao wamepatiwa chanjo hiyo kituo cha afya makambako wamesema bado kuna dhana potofu katika jamii kuhusiana na chanjo ya surua ndio maana wengi wao wanashindwa kuwapeleka watoto wao wapate chanjo.
Watoto 13,146 wamelengwa kufikiwa na chanjo hiyo katika Halmshauri ya Mji wa Makambako.