CRB,ERB zamshukia Mkandarasi

DODOMA-Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB), na Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB), zimetoa onyo kali kwa Mkandarasi ECIA Company Ltd, anayejenga barabara ya Kanyinabushwa-Mbale “A” wilayani Misenyi mkoani Kagera kutokana na kutozingatia kanuni, sheria na miongozo ya shughuli za majenzi nchini.
Akizungumza na vyombo vya Habari Jijini Dodoma, Msajili wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi Mha. Rhoben Nkori, amesema timu ya pamoja ya CRB na ERB baada ya kuchunguza ujenzi wa Kalvati lililobomoka kabla ya ujenzi wake kukamilika imebaini kuwa uharibifu huo ulisababishwa na matumizi ya malighafi hafifu kinyume cha matakwa ya mkataba na kuruhusu kupita kwa vyombo vya moto katika barabara hiyo kabla ya Kalvati lililojengwa kukamilika.

“Kwa mujibu wa sharia ya usajili wa mkandarasi sura ya 35 ya mwaka 2002 tumempa onyo kali Mkandarasi ECIA Company Limited na endapo akirudia tena kosa la aina hiyo atachukuliwa hatua kali zaidi”, alisema Mha. Nkori.

Naye Msajili wa Bodi ya Wahandisi Mha. Benard Kavishe amesema ERB inawataka wakandarasi wote wahakikishe wanaajiri wahandisi wenye sifa ili kusimamia miradi kikamilifu na hivyo kuleta usalama kwa watumiaji.

Amesema kwa mujibu ya sharia ya Usajli wa wahandisi Sura ya 63 ya mwaka 2012 ni kosa kwa mtu asiyekua na taaluma ya uhandisi na asiyesajiliwa na bodi ya usajili ya wahandisi kutojihusisha na shughuli za kihandisi.

“Tunatoa wito kwa wananchi na wakandarasi wote nchini, kuhakikisha kuwa shughuli zote za ujenzi zinasimamiwa na wataalamu wenye weledi na waliosajiliwa ili kuleta tija na ufanisi, na wote watakaobainika kukiuka sheria hizo Bodi haitosita kuwachukulia hatua za kisheria”, amesema Mha. Kavishe.

Uchunguzi huo unafuatia maelekezo yaliyotolewa na Waziri wa Ujenzi Mhe. Innocent Bashungwa Januari 17 mwaka huu kufuatia kadhia ya kubomoka kwa kalvati katika barabara ya Kanyinabushwa-Mbale “A” Wilayani Misenyi Mkoani Kagera.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news