DCEA yawapa walimu,wanafunzi elimu kuhusu dawa za kulevya

DODOMA-Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) Kanda ya Kati, tarehe 21 Februari, 2024 imetoa elimu ya dawa za kulevya kwa walimu 14 na wanafunzi 630 wa shule ya msingi Mnyakongo iliyopo jijini Dodoma.
Chini ya uongozi mahiri wa Kamishna Jenerali Aretas Lyimo, watumishi wa mamlaka hiyo wamekuwa mstari wa mbele kuhakikisha wanaendelea kutekeleza majukumu yao kwa weledi na ufanisi wa hali ya juu ili kuhakikisha dawa za kulevya hazipati nafasi nchini.
Pia, elimu iliyotolewa shuleni hapo ni mwendelezo wa hatua mbalimbali zinazochukuliwa na mamlaka kuhakikisha elimu kuhusu dawa za kulevya inayafikia makundi mbalimbali ya jamii wakiwemo wanafunzi nchini kote. 

Dhamira kuu ikiwa ni kuwapa uelewa wa kutosha ambao utawawezesha kujiepusha kujihusisha na biashara au matumizi ya dawa za kulevya waweze kutimiza ndoto zao.
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) ilianzishwa chini ya kifungu cha 3 cha Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Na. 5 ya Mwaka 2015.

Sheria hii iliifuta Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya. Kuanzishwa kwa Mamlaka Kulitokana na mapungufu yaliyokuwepo katika mfumo wa udhibiti wa dawa za kulevya.

Mapungufu hayo yalikuwa ni pamoja na Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya iliyoanzishwa na Sheria ya ya Kuzuia Biashara Haramu ya Dawa za Kulevya Namba 9 ya mwaka 1995 kukosa nguvu ya kisheria ya kupeleleza, kufanya uchunguzi na kukamata wahalifu wa dawa za kulevya.
Kutokana na mapungufu hayo, Baraza la Mawaziri katika kikao chake cha tarehe 8 Novemba, 2007 (Waraka Na 60/2007) liliagiza, kurekebisha au kufuta Sheria ya Kuzuia Biashara Haramu ya Dawa za Kulevya Namba 9 ya mwaka 1995.

Ni ili kukidhi matakwa na changamoto za udhibiti wa matumizi na biashara ya dawa za kulevya. Baraza la Mawaziri liliagiza kuundwa kwa chombo cha kupambana na dawa za kulevya chenye uwezo kiutendaji kwa kukipa mamlaka ya ukamataji, upekuzi na upelelezi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola ili kuongeza ufanisi wa udhibiti wa dawa za kulevya nchini.

Kufuatia agizo hilo, tarehe 24/03/2015 Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilitunga na kupitisha Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Na. 5 ya Mwaka 2015 na kuanza kutumika rasmi tarehe 15 Septemba, 2015 kupitia tangazo la Serikali namba 407 (GN NO.407/2015).

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ilianza kutekeleza majukumu yake kikamilifu tarehe 17 Februari, 2017 baada Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kumteua Kamishna Jenerali.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news